2014-08-12 09:02:15

Wakristo wanatafuta hifadhi katika mazingira magumu na hatarishi!


Kardinali Leonardo Sandri, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa kwa ajili ya Makanisa ya Mashariki anamshukuru Baba Mtakatifu Francisko kwa kujali mateso na mahangaiko ya Wakristo huko Iraq ambao wamelazimika kuyakimbia makazi yao kwa kuhofia usalama wa maisha yao. Wakristo hawa wanatafuta hifadhi katika hali na mazingira magumu, hili ni jambo ambalo linawatia watu wengi simanzi.

Kardinali Sandri anapenda kuungana na Baba Mtakatifu pamoja na Watu wote wenye mapenzi mema ili kuwaombea Wakristo huko Iraq, ili waweze kupata faraja na mshikamano kutokana kwa watu wenye mapenzi mema, wakati huu wa majaribio makubwa, yanayogusa undani wa utu na heshima yao kama binadamu.

Ni matumaini ya Kardinali Sandri kwamba, viongozi wa Jumuiya ya Kimataifa na watu wote wenye mapenzi mema wataguswa na mahangaiko ya watu wanaoishi huko Iraq na Syria, maeneo ambayo kwa sasa yamekumbwa na vita inayoendelea kusababisha majanga makubwa kwa watu na mali zao.

Wakristo nchini Iraq, wamekuwepo huko kwa takribani miaka elfu mbili iliyopita, leo hii kuwafukuza na kuwalazimisha kuyakimbia makazi yao ni jambo ambalo haliwezi kukubalika na wengi, huu ni unyanyasaji na madhulumu ya kidini.

Baraza la Kipapa la Makanisa ya Mashariki linasema, kwa sasa linaendelea kuwasiliana kwa karibu na viongozi wakuu wa Makanisa huko Mashariki ya Kati pamoja na wawakilishi wa Vatican walioko huko Mashariki ya Kati, ili kupanga mikakati ya kuwasaidia watu wanaoteseka kutokana na vita na kinzani za kijamii. Kuna wasi wasi kwamba, vita hii ikageuka kuwa ni mauaji ya kimbari dhidi ya Wakristo huko Iraq.








All the contents on this site are copyrighted ©.