2014-08-12 11:36:46

Waamini walei ni nguzo ya Kanisa Katoliki nchini Korea!


Baba Mtakatifu Francisko anaanza hija yake ya kitume nchini Korea inayoongozwa na kauli mbiu "Ondoka, uangaze, kwa kuwa nuru yako imekuja, na utukufu wa Bwana umekuzukia". Akiwa nchini Korea, Baba Mtakatifu anatarajiwa kukutana na umati mkubwa wa waamini walei ambao kwa miaka mingi wameendelea kujisadaka kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya Kanisa.

Baraza la Maaskofu Katoliki Korea ya Kusini linatambua na kuthamini mchango unaotolewa na waamini walei ndiyo maana, linaendelea kutoa kipaumbele cha kwanza kwa majiundo awali na endelevu kwa waamini wa Kanisa Katoliki nchini Korea, ili kweli waweze kuwa ni chumvi na mwanga, unaoweza kuyatakatifuza malimwengu.

Kanisa Katoliki nchini Korea bado ni changa na katika uchanga wake, linataka kuendelea kukua na kukomaa kwa kujikita katika imani tendaji inayojidhihirisha katika uhalisia wa maisha. Waamini walei daima wameonesha ile kiu ya kutaka kuyafahamu Mafundisho Tanzu ya Kanisa, ili waweze kuwa karibu zaidi na Mwenyezi Mungu.

Wanawaomba Maaskofu wawapatie Katekesi ya kina kuhusu maadhimisho ya Sakramenti za Kanisa ili kweli, Sakramenti hizi ziwajalie neema na baraka katika maisha yao. Wanataka kuzifahamu Amri za Mungu, ili ziwe ni dira na mwongozo wa maisha, ili hatimaye, wawe kweli ni Wachamungu wanaomwilisha imani yao katika matendo adili na manyofu.

Waamini walei nchini Korea ya Kusini wanasema, hata wao kama walivyo waamini wengine wanakabiliwa na changamoto mbali mbali za maisha kama vile: ukosefu wa fursa za ajira, kuyumba kwa tunu msingi za maisha ya ndoa na familia; kuporomoka kwa maadili, changamoto ambazo zinapaswa kufanyiwa kazi kwa katekesi makini na endelevu, kazi inayofanywa na Jumuiya ndogo ndogo za Kikristo.

Wafiadini 124 watakaotangazwa kuwa Wenyeheri ni kielelezo cha dhamana na utume wa waamini walei katika kuyatakatifuza malimwengu. Hawa ni mfano wa kuigwa na waamini walei, sehemu mbali mbali za dunia.







All the contents on this site are copyrighted ©.