2014-08-12 09:28:42

Simameni kidete kulinda na kutetea taasisi ya familia!


Wajumbe wa kongamano la familia kimataifa lililoadhimishwa hivi karibuni nchini Ufilippini katika hati yao ya mwisho wanasema kwamba, mustakabali na ustawi wa watu Barani Asia una uhusiano mkubwa na familia. RealAudioMP3

Kutokana na changamoto hii, Serikali Barani Asia pamoja na Kanisa kwa kushirikiana na watu wote wenye mapenzi mema hawana budi kukuza na kuendeleza taasisi ya ndoa na familia ambayo kwa sasa inakabiliana na changamoto nyingi kutoka ndani na nje ya familia yenyewe!

Kongamano hili liliandaliwa na Baraza la Maaskofu wa Kanisa Katoliki Ufilippini kwa kushirikiana na Baraza la Kipapa la Familia, kwa kuongozwa na kauli mbiu “Familia Barani Asia, mwanga wa matumaini”. Kongamano hili lilikuwa ni sehemu ya maadhimisho ya kumbu kumbu ya miaka 30 ya Waraka wa Haki Msingi za Mtoto iliyotolewa na Baraza la Kipapa la Familia baada ya maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kuhusu familia, iliyoadhimishwa mjini Vatican kunako mwaka 1980.

Waraka huu unabainisha pamoja na mambo mengine haki msingi za familia inayojikita katika ndoa kati ya Bwana na Bibi kadiri ya mpango wa Mungu. Kongamano hili limeadhimishwa kwa wakati muafaka kwani Mama Kanisa anajiandaa kuadhimisha Sinodi maalum ya Maaskofu kwa ajili ya familia mwezi Oktoba 2014 mjini Vatican ili kufanya upembuzi yakinifu kuhusu fursa, matatizo na changamoto zinazoendelea kujitokeza katika maisha ya ndoa na familia, ili kwa pamoja, Mababa wa Sinodi waweze kuibua mbinu mkakati wa kichungaji utakaotumiwa na Makanisa mahalia, kama kielelezo cha umoja na mshikamano wa Kanisa.

Wajumbe wa kongamano hili huko Manila, Ufilippini walipinga kwa nguvu zote kuhusu utamaduni wa kifo unaojitokeza katika sera za utoaji mimba kwa kisingizio cha afya ya uzazi salama. Kanisa linaendelea kufundisha umuhimu wa tunu msingi za maisha ya ndoa na familia kama msingi thabiti wa jamii.

Wajumbe wanasema, katika kipindi cha miaka hamsini iliyopita, kumekuwepo na mabadiliko makubwa sana duniani katika sekta mbali mbali za maisha: kiuchumi, kijamii, kisiasa, kitamaduni na hata kidini. Mabadiliko yote haya yameielemea Familia ya binadamu kwa kiasi kikubwa, ingawa familia zenyewe ndizo zilizokuwa chanzo cha mabadiliko haya na muathirika mkubwa wa changamoto zinazoendelea kujitokeza katika ulimwengu mamboleo.

Wajumbe wanasema, leo hii kuna watu duniani wanadai ndoa za jinsia moja, jambo linalokwenda kinyume cha mpango wa Mungu, utu na heshima ya binadamu; sera za utoaji na vizuia mimba limeendelea kuwa ni sehemu ya utamaduni mamboleo bila kusahau umaskini, njaa na magonjwa yanayoendelea kuwaandama mamillioni ya watu duniani.

Umaskini na hali ngumu ya maisha ni mbolea inayostawisha biashara haramu ya binadamu, utalii wa ngono na picha chafu kwenye mitandao pamoja na mifumo mbali mbali inayofumbatwa katika utumwa mamboleo.

Mambo yote haya yanadhalilisha utu na heshima ya binadamu. Baadhi ya Serikali zimekuwa na sera tenge kwa tunu msingi za maisha ya ndoa na familia na matokeo yake zinashiriki katika kuziandama familia. Pale ambapo familia inashambuliwa, ikumbukwe kwamba, hata mustakabali wa binadamu uko mashakani!








All the contents on this site are copyrighted ©.