2014-08-12 09:16:53

Juhudi za Baraza la Makanisa Ulimwenguni katika mchakato wa kudumisha haki na amani


Baraza la Makanisa Ulimwenguni katika mkutano wake wa hivi karibuni limebainisha kwamba, bado kuna kinzani, migogoro na vita sehemu mbali mbali za dunia, kama inavyojionesha huko Mashariki ya Kati, Sudan ya Kusini, Nigeria na Ukrain. RealAudioMP3

Licha ya kinzani zote hizi, Kanisa bado limeendelea kujielekeza zaidi katika kutafuta: haki, amani na utulivu. Baraza la Makanisa linatambua dhamana hii kama sehemu ya utekelezaji wa changamoto zilizotolewa kwenye mkutano mkuu wa kumi wa Baraza hili ulioadhimishwa huko Busan, Korea ya Kusini, kunako mwaka 2013.

Kwa sasa Makanisa yako kwenye hija ya haki na amani. Makanisa hayana budi kutafuta njia ambazo zitasaidia kulinda na kudumisha haki, amani na utulivu sanjari na kutafuta mikakati ya kukomesha mambo yanayopelekea uvunjwaji wa haki msingi za binadamu. Kwa mfano kusitisha vita Sudan ya Kusini ni jambo muhimu sana na linapaswa kupewa kipaumbele cha kwanza, lakini pia kuna haja ya kutafuta dawa itakayoweza kudumisha amani katika mazingira ambamo hakuna uhuru wa kweli, hakuna fursa za ajira; ukweli na matumaini kwa watu wengi yanatoweka kama ndoto ya mchana!

Zote hizi ni ndago zinazoweza kuchochea kinzani, vurugu na hatimaye vita. Makanisa na vyama vya kiraia nchini Sudan ya Kusini vimekuwa vikiitaka Serikali iliyoko madarakani kusaidia mchakato wa kuleta mageuzi yatakayosaidia kulinda na kudumisha misingi ya haki na amani, lakini bila mafanikio. Jambo la kwanza lilikuwa ni kuwanyang’anya silaha wale wote wanaomiliki silaha kinyume cha sheria na hapo kuanza hatua ya pili inayojielekeza zaidi katika upatanisho wa kitaifa unaokumbatia utawala bora.

Kwa miaka mingi, Baraza la Makanisa Ulimwenguni limejitahidi kadiri ya uwezo wake kuwahamasisha viongozi wa Korea ya Kusini na Kaskazini, kuanza mchakato wa upatanisho ili kuweza kujenga umoja wa kitaifa kati ya nchi hizi pacha, ambazo zilijikakamua kutafuta uhuru wake baada ya kutawaliwa na Japan kwa mkono wa chuma na Japan kwa kipindi cha miaka thelathini na sita.

Lakini, jambo la kusikitisha ni kuona kwamba, bado Korea imegawanyika kutokana na vita vilivyotimua vumbi kunako mwaka 1950 na hivyo kusababisha maafa makubwa kwa wananchi wa pande hizi mbili. Umoja wa kitaifa hautawezekana bila ya amani na hakuna amani ya kudumu bila ya kuanza mchakato wa upatanisho wa kitaifa na kwamba, upatanisho unaweza kuzaa matunda yanayokusudiwa ikiwa kama msamaha utapatikana. Hapa kuna mchezo mchafu unaofanywa na mataifa makubwa kwa ajili ya masilahi ya nchi husika. Itakumbukwa kwamba, tarehe 25 Agosti 2014, Baraza la Makanisa Ulimwenguni litafanya ibada maalum kwa ajilu ya kuombea umoja na mshikamano wa kitaifa kati ya Korea hizi mbili.

Vitendo vya kigaidi vinavyofanywa na kikundi cha kigaidi cha Boko Haram ndani na nje ya Nigeria vimepelekea idadi kubwa ya watu kulazimika kuyakimbia makazi kwa kuhofia usalama wa maisha yao na kwamba, walengwa wakuu ni Wakristo wanaoishi Kaskazini mwa Nigeria, ingawa hata waamini wa dini nyingine pia wanashambuliwa. Kadiri ya takwimu za kimataifa zinaonesha kwamba, kuna zaidi ya watu 3, 000 ambao wameuwawa kinyama na Boko Haram nchini Nigeria hadi sasa.

Wasichana 250 waliotekwa nyara na Boko Haram bado hawajahachiliwa huru na hatima yao haijulijkani. Vitendo vyote hivi vinadhalilisha maisha, utu na heshima ya binadamu na kwamba, Jumuiya ya Kimataifa haina budi kusimama kidete kulinda na kutetea utu na heshima ya binadamu pamoja na uhuru wa kuabudu.








All the contents on this site are copyrighted ©.