2014-08-11 10:38:24

Watu wanalilia amani duniani na wala si vita!


Mke wa Waziri mkuu wa Tanzania, Mama Tunu Pinda amesema wanawake wote duniani wanalilia amani na hawapendi vita wala machafuko kwani husababisha amani kutoweka kwenye familia na vifo vya watu wasio na hatia. Ametoa wito huo Jumapili, Agosti 10, 2014 wakati akitoa mada kama mzungumzaji mkuu kwenye Mkutano wa Dunia wa siku tano ulioanza Jumapili jijini Seoul, Korea Kusini.
Mkutano huo ambao umeandaliwa na taasisi ya Universal Peace Federation (UPF) ambayo inatoa ushauri kwenye Baraza la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia masuala ya Uchumi na Kijamii unajadili masuala ya Amani, Usalama na Maendeleo.
Akiwasilisha mada yake kuhusu usalama, amani na maendeleo barani Afrika, Mama Tunu Pinda alisema: “Ninaiomba jamii ya Kimataifa duniani kote tusimamie amani na usalama kwani kinyume na hapo ni kuleta machafuko na vita. Wanawake hatupendi vita wala machafuko...,” alisema huku akishangiliwa.
Aliwataka washiriki wa mkutano huo wasimame katika nafasi zao kama baba na mama, kama kaka na dada na kuhakikisha kuwa dunia inakuwa ni mahali pazuri pa kuishi. “Ninawasihi tuendeleze maono ya Muumba wetu, tuweke utu mbele kwa kuwajali wengine na tuache kutanguliza maslahi yetu binafsi,” alisema.
Mapema, akiwakaribisha wajumbe zaidi ya 500 kutoka nchi 68 wanaoshiriki mkutano huo, Rais wa UPF, Dk. Thomas Walsh alisema taasisi hiyo inasimamia misingi ya amani, usalama na maendeleo ya jamii kwa nia ya kujenga umoja na mshikamano miongoni mwa mataifa mbalimbali.
Alisema anatumaini uwepo wa wakuu wa nchi mbalimbali na viongozi mashuhuri, utasaidia kupata majibu ya changamoto inayoikabili dunia juu ya upatikanaji wa amani ya kudumu.
Naye, Mfalme Letsie Mswati III kutoka Lesotho, akizungumza katika mkutano huo alisema dunia inakabiliwa na changamoto nyingi za ukosefu wa amani kubwa ikiwa ni uharibifu wa mazingira. Aliwataka wajumbe wa mkutano huo kuhakikisha wanahimiza utunzaji wa mazingira kama njia ya kupunguza matatizo yanayojikeza kutokana na mabadiliko ya tabianchi.
Alionya kwamba kuna haja ya kuweka mifumo madhubuti ya kuhakikisha kuwa dunia haiendelei kuwa na matukio ya kigaidi na matumizi ya silaha za maangamizi. “Kama tutakubali vita viendelee kutokea, na migogoro isiyokwisha barani Afrika na nchi za Uarabuni, ni lazima tukubali kuwa hakutakuwa na maendeleo katika mabara haya,” alisema.








All the contents on this site are copyrighted ©.