Papa Francisko anaguswa na mateso ya wananchi wa Iraq
Baba Mtakatifu Francisko wakati wa sala ya Malaika wa Bwana, Jumapili tarehe 10 Agosti
2014 kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro alitangaza kwamba, amemteua Kardinali
Fernando Filoni, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la uinjilishaji wa watu kumwalikisha
rasmi nchini Iraq, kama kielelezo cha mshikamano wa dhati na wananchi wa Iraq ambao
kwa sasa wanakabiliwa na majanga makubwa!
Baba Mtakatifu Jumapili jioni alikutana
na kuzungumza na Kardinali Filoni kuhusu undani wa ziara yake nchini Iraq. Baba Mtakatifu
ameonesha masikitiko yake makubwa kutokana na mateso na mahangaiko ya wananchi wa
Iraq. Ametoa kiasi cha fedha kwa ajili ya kuwasaidia wananchi wa Iraq ambao kwa sasa
wanakabiliwa na mahitaji makubwa, kama kielelezo makini cha mshikamano wake na Jumuiya
ya Kimataifa inayoendelea pia kutoa msaada wa hali na mali.
Kardinali Filoni
katika mahojiano na Kituo cha Televisheni cha Vatican kabla ya kuondoka mjini Vatican
siku ya Jumatatu kuelekea Iraq anasema kwamba, Baba Mtakatifu ameguswa sana na mahangaiko
ya wananchi wa Iraq, pengine alitamani kuwepo mwenyewe ili kuonesha mshikamano wake,
lakini dhamana hii amempatia Kardinali Filoni. Watu wanaoteseka na kuhangaika ndio
maskini wa nyakati hizi wanaopaswa kuhudumiwa kikamilifu.
Kardinali Filoni
anasema, utume wake nchini Iraq inapania kuwatia shime, imani na matumaini, ili kwamba,
licha ya mateso na madhulumu wanayokabiliana nayo wasikate tamaa bado waendelee kutambua
kwamba, Iraq ni nchi ambayo ina utajiri mkubwa ambao kwa miaka mingi umewasaidia wananchi
wa dini mbali mbali kuishi kwa amani na utulivu. Inasikitisha kuona kwamba, baadhi
ya watu wanataka kuupoteza utajiri huu.
Hii ni hija ta matumaini kwamba, bado
kuna matumaini ya kesho iliyo bora zaidi na kwamba, Kanisa la Kiulimwengu liko pamoja
nao. Baba Mtakatifu anapenda kuwahimiza waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi
mema kuwasaidia wananchi wa Iraq.