2014-08-11 09:16:24

Mshikamano wa dhati na Wakristo Mashariki ya Kati!


Baraza la Maaskofu Katoliki Canada linasema kwamba, kuna haja kwa Jumuiya ya Kimataifa kwa kushirikiana na watu wenye mapenzi mema, kuwasaidia wananchi wa Iraq ambao kwa sasa wanakabiliwa na majanga makubwa katika maisha. Vita inayoendelea huko Mashariki ya Kati ni hatari kwa usalama, ustawi na mafao aya wengi. Vita nchini Iraq, Ukanda wa Ghaza na Syria ni changamoto kwa Jumuiya ya Kimataifa kuhakikisha kwamba, watu wanaheshimu uhuru wa kuabudu, haki za makundi madogo pamoja na haki msingi za binadamu.

Huu ni wajibu msingi kwa viongozi wa Serikali. Maaskofu Katoliki Canada wanaiomba serikali yao kutengenga nafasi kwa ajili ya kuwapokea wananchi kutoka Iraq wanaokimbia vita ili kusalimisha maisha yao na kwamba, Jimbo kuu la Canada liko tayari kupokea baadhi ya wakimbizi na kuwapatia hifadhi katika taasisi zake.

Jumapili iliyopita, tarehe 10 Agosti 2014, Waamini wa dini mbali mbali wameandamana kwa ajili ya kuombea amani na utulivu huko Mashariki ya Kati. Tarehe 17 Agosti 2014 katika Madhabau ya Sakramenti kuu, Jimbo kuu la Quebec, kutakuwa na Maadhimisho ya Ibada ya Misa takatifu kwa ajili ya kuombea amani na mshikamano huko Iraq na Mashariki ya Kati.

Nia ya Ibada ya Misa ni kwa ajili ya wahanga wa vita sehemu mbali mbali za dunia. Tarehe 4 Oktoba 2014 kutafanyika Ibada ya pamoja kwa waamini wa Madhehebu mbali mbali ya Kikristo kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Paulo, Jimbo kuu la Toronto na baadaye kutafanyika Ibada ya Misa Takatifu.

Wakati huo huo, Baraza la Maaskofu Katoliki Marekani linaendelea kukusanya misaada mbali mbali kwa ajili ya kuwasaidia wananchi walioko Mashariki ya Kati. Wakristo pamoja na watu wote wenye mapenzi mema wanahimizwa kuonesha mshikamano wao wa dhati na wananchi wanaoteseka na kudhulumiwa kutokana na imani yao kwa Kristo na Kanisa lake.

Tarehe 17 Agosti 2014, Baraza la Maaskpofu Katoliki Marekani linawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kusali kwa ajili ya kuombea amani duniani.








All the contents on this site are copyrighted ©.