Matumaini ya Kanisa Katoliki nchini Korea ya Kusini
Baraza la Maaskofu Katoliki Korea kwa namna ya pekee kabisa linapenda kumshukuru Baba
Mtakatifu Francisko kwa kuonesha moyo wa ujasiri na utashi wa kutembelea Korea, cheche
ya matumaini katika mchakato wa upatanisho wa kitaifa kati ya Korea ya Kusini na Korea
ya Kaskazini. Ni hija inayopania kuwaimarisha ndugu zake katika imani. Ni maneno ya
Askofu Peter U-ill Kang, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Korea katika mahojiano
maaluma na Shirika la Habari la UCANEWS.
Korea ilijikuta inagawanyika na kuwa
ni nchi mbili tofauti kunako mwaka 1945, lakini bado ni watu wanaozungumza lugha moja
wakiwa wameshikamana na utamaduni wao na kwamba, dalili zinaonesha kuwa utengano huu
hautakuwa wa muda mrefu, kwani alama za nyakati zinaonesha kwamba, watu wanataka umoja
na mshikamano wa kitaifa. Mabadiliko msingi hayana budi kuchomoza kutoka ndani ya
nchi husika na hadi sasa kuna cheche za mabadiliko zinazoendelea kujitokeza siku hadi
siku, hasa Korea ya Kaskazini.
Wananchi wengi wa Korea ya Kaskazini wanakabiliwa
na hali ngumu ya maisha kiasi kwamba, uvumilivu wao kwa sasa unaonekana kufikia ukomo.
Baa la njaa kati ya watu ni chachu ya mapinduzi ya kisiasa na kijamii, ili kujikita
katika mchakato wa kukuza na kudumisha haki ya kweli na demokrasia kwa ajili ya ustawi
na maendeleo ya wengi.
Askofu Peter anasema, hata ndani ya Kanisa lenyewe kuna
mpasuko unaojionesha kwani kuna baadhi ya Makleri wanaounga mkono Serikali na wengine
wako kinyume cha utawala wa mabavu, hapa Kanisa linajikutalikiwa njia panda katika
utekelezaji wa maisha na utume wake katika jamii. Mpasuko huu hauna uhusiano wowote
na masuala ya Mafundisho tanzu ya Kanisa.
Ukosefu wa haki jamii ni kati ya
changamoto zinazowakabili vijana wengi Korea ya Kusini, Kanisa kwa kujikita katika
Mafundisho Jamii linapenda kuwapatia vijana matumaini kwa leo na kesho iliyo bora
zaidi, lakini hili ni jambo linalohitaji muda na rasilimali nyingi.