2014-08-11 09:10:58

Hali halisi ya maisha na utume wa Kanisa Korea ya Kusini


Takwimu zilizotolewa na Baraza la Maaskofu Katoliki Korea ya Kusini kwa mwaka 2013 zinaonesha kwamba, idadi ya Waamini wa Kanisa Katoliki nchini humo imendelea kuongezeka maradufu katika kipindi cha miaka kumi iliyopita. Kuna Wakristo million 5.5 katika nchi yenye raia wapatao million 50. Idadi ya Wakatoliki nchini Korea ya Kusini imeongezeka kwa asilimia 1.5% katika kipindi cha mwaka uliopita. RealAudioMP3

Hii ndiyo hali ambayo Baba Mtakatifu Francisko anatarajiwa kukutana nayo wakati wa hija yake ya kitume Nchini Korea ya Kusini, ili kushiriki katika maadhimisho ya Siku ya Sita ya Vijana Barani Asia pamoja na kuwatangaza Watumishi wa Mungu kutoka Korea kuwa ni Wenyeheri. Pamoja na mafanikio yote haya, Maaskofu wanasema, idadi ya waamini wanaohudhuria Ibada ya Misa takatifu kila jumapili imepungua na kwamba, ndoa nyingi zinayumba kutokana na kumezwa mno na malimwengu pamoja na athari za utandawazi.

Kanisa Katoliki nchini Korea ya Kusini lina jumla ya Mapadre 4, 901 na kati yao kuna Mapadre Wamissionari 173. Takwimu zinaonesha kwamba, Mapadre wa Jimbo ni 3, 995 na Mapadre Watawa ni 697 na Mapadre Wamissionari 173. Kuna jumla ya watawa 10, 173. Idadi ya Wakatoliki waliofunga ndoa kwa mwaka 2013 ilikuwa ni Wakatoliki 19,424 pungufu ya asilimia 6. 2% ikilinganishwa na Wakatoliki waliofunga ndoa kwa mwaka 2012.

Licha ya changamoto hizi za kichungaji zinazoendelea kujitokeza nchini Korea ya Kusini, lakini Kanisa linajivunia kwa kiasi kikubwa ukomavu wa Jumuiya ndogo ndogo za Kikristo, nyenzo msingi ya Uinjilishaji kwa Makanisa Barani Asia, Amerika ya Kusini na Afrika. Jumuiya ndogo ndogo za Kikristo ndiyo nguzo ya Kanisa Korea ya Kusini na kwa kipindi cha miaka ishirini Baraza la Maaskofu Katoliki Korea limejielekeza zaidi katika kukuza na kuimarisha Jumuiya ndogo ndogo za Kikristo kama chombo kikuu cha Uinjilishaji, mahali ambapo waamini wanapata fursa ya kusikiliza, kutafakari na kumwilisha Neno la Mungu kadiri ya mahitaji na mazingira yao.

Hii imekuwa ni shule makini ya kukuza na kuimarisha maisha ya Kisakramenti pamoja na kuendeleza mshikamano wa udugu na upendo ndani ya Kanisa. Kwa kutambua umuhimu na mchango wa Jumuiya ndogo ndogo za Kikristo, Baraza la Maaskofu Katoliki Korea ya Kusini limechapisha mwongozo wa kufuata ili kuimarisha Jumuiya ndogo ndogo za Kikristo nchini humo.








All the contents on this site are copyrighted ©.