2014-08-09 09:40:39

Rais Mutharika wa Malawi amemwalika Rais Kikwete wa Tanzania kwenda kutembelea Malawi, ili kula samaki Ziwa Nyasa!


Rais Jakaya Mrisho Kikwete wa Tanzania, Jumatano, Agosti 6, 2014, alikutana na kufanya mazungumzo na Rais mpya wa Malawi, Mheshimiwa Peter Mutharika, mazungumzo yaliyofanyika katika mazingira ya udugu na urafiki.

Viongozi hao wawili walikutana kwenye Hoteli ya Ritz Carlton, Georgetown, Washington D.C., ambako viongozi hao wawili walikuwa wamefikia wakati wanahudhuria Mkutano wa Viongozi wa Nchi za Marekani na Afrika ambao ulimalizika tayari na ulikuwa unafanyika katika Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani chini ya uenyekiti wa Rais Barack Obama wa Marekani.

Rais Mutharika ambaye aliapishwa kuwa Rais wa Malawi Mei 30, mwaka huu, 2014, alimwalika Rais Kikwete kutembelea Malawi kutembelea “ndugu zako wa Malawi, Sisi sote ni ndugu, ni watu wamoja, tuna uhusiano wa karibu na wa miaka mingi na makabila yetu yako kila upande wa mpaka wetu.”

Akizungumza mbele ya mke wake na Mama Salma Kikwete ambao nao walifanya mazungumzo ya kwao mbali na yake na marais, Rais Mutharika alisema: “Kama mnavyojua, Tanzania mimi ni nyumbani kwangu, na niliondoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam hata kabla ya Mheshimiwa Rais Kikwete hajajiunga na chuo hicho.”

Kuhusu mwaliko wa kumwomba Rais Kikwete kutembelea Malawi,Rais Mutharika amesema: “Nataka uje tumpumzike kwenye Ziwa (Ziwa Nyasa) na tule samaki pamoja. Tuna samaki watamu sana” Rais Mutharika pia alimwambia Rais Kikwete kuwa hata kama mpaka sasa hajapata muda wa kuja Tanzania kujitambulisha, kama ilivyo jadi ya marais wapya wa ukanda wa Jumuia ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC).

“Niliingia madarakani katika mazingira magumu kidogo na sijaweza kupata nafasi ya kupumua ili niweze kutembelea nchi za jirani,” Rais Mutharika amemwambia Rais Kikwete katika mazungumzo ambayo pia yalihudhuriwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mheshimiwa Bernard Membe.

Rais Kikwete amemshukuru Rais Mutharika kwa mwaliko huo akimweleza kuwa hakuweza kufika kwenye sherehe ya kuapishwa kwake kuwa Kiongozi wa Malawi kwa sababu ya muda mfupi kati ya kutangazwa mshindi na kuapishwa.
“Kwa niaba ya Watanzania, napenda kukupongeza Mheshimiwa Rais kwa ushindi na heshima kubwa ambayo wananchi wa Malawi wamekupa kwa kukuchagua kuwa Rais wao.”

Makamu wa Rais, Dkt. Mohamed Gharib Bilal ndiye aliiwakilisha Tanzania na Rais Kikwete kwenye sherehe za kuapishwa kwa Rais Mutharika. Rais Mutharika pia ametumia nafasi hiyo ya kukutana na Mheshimiwa Rais Kikwete kumwelezea maendeleo ya kisiasa na kiuchumi katika nchi hiyo rafiki na jirani ya Malawi na changamoto zinazoukabili uongozi wake mpya.

Wakati huo huo, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete Alhamisi, Agosti 7, 2014, amekutana na kufanya mazungumzo ya faragha na Rais wa 43 wa Marekani, George W. Bush mjini Dallas, Jimbo la Texas, katika siku ya nane ya ziara yake ya siku tisa nchini Marekani.

Aidha, Rais Kikwete ametembelea Maktaba ya Kirais ya Rais Bush – Bush Presidential Library- na kujionea mwenyewe nafasi kubwa iliyotolewa kwa Tanzania na zawadi ambazo Rais Bush alizipata katika ziara yake rasmi ya Tanzania wakati akiwa Rais wa Marekani. Rais Kikwete amejionea mwenyewe Maktaba hiyo ya kuvutia sana na inayoendeshwa kwa teknolojia ya kisasa kabisa ya habari na mawasiliano.

Rais Kikwete amesimama mjini Dallas akiwa njiani kutoka Washington D.C., kwenda Houston, jimbo hilo hilo la Texas kuhudhuria mkutano wa wafanyabiashara wa mafuta na gesi ambao wanataka kuwekeza katika sekta hiyo katika Tanzania.
Rais Kikwete amekuwa katika Marekani kwa ziara ya kikazi ya siku tisa, ambako miongoni mwa mambo mengine, amehudhuria Mkutano wa Wakuu wa Nchi za Marekani na Afrika uliofikia kilele chake jana kwa kikao kilichoendeshwa na Rais Barack Obama wa Marekani katika Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani mjini Washington D.C.

Kwenye Maktaba hiyo ya Rais George W. Bush, Rais Kikwete ambaye ameambatana na Mama Salma Kikwete amejionea mwenyewe nafasi kubwa iliyotolewa kwa Tanzania na Kiongozi huyo wa Marekani ambaye alifanya ziara rasmi ya siku nne nchini Tanzania mwezi Februari 2008.

Miongoni mwa zawadi ambazo Rais Bush alipewa Tanzania na ziko katika Maktaba hiyo ni pamoja na Simba mkubwa ambaye ni kivutio kikubwa cha watu na watalii wanaotembelea Maktaba hiyo pamoja na seti ya mkufu wa madini ya Tanzanite ambao alipewa Mama Bush wakati wa ziara hiyo na Mama Salma Kikwete.
Zawadi nyingine kutoka Tanzania kwenye Maktaba hiyo ni pamoja na Biblia ya Kiswahili, kanga ya kumbukumbu ya ziara rasmi ya Rais mstaafu Bush na Mama Laura Bush nchini Tanzania, shanga na mgolole wa Kabila la Wamasai.








All the contents on this site are copyrighted ©.