Korea ya Kusini inaendelea kuwekeza katika majadiliano ya kiekumene!
Kuanzishwa kwa Tume ya Kiekumene ya Imani na Katiba kunako tarehe 22 Mei 2014 nchini
Korea ya Kusini imekuwa ni hatua kubwa katika mchakato wa majadiliano ya kiekumene
kati ya Makanisa nchini humo. Haya ni matunda ya ushirikiano wa miaka mingi baina
ya Makanisa na kwamba, kwa sasa wanasubiri kwa hamu kubwa hija ya kichungaji ya Baba
Mtakatifu Francisko, ili kuvuka vikwazo vilivyopitwa na wakati tayari kuanza mwelekeo
mpya wa majadiliano ya kiekumene.
Kanisa Katoliki nchini Korea ya Kusini linapenda
kujielekeza zaidi na zaidi katika kukuza na kuimarisha mchakato wa upatanisho wa kitaifa,
haki na amani mintarafu utangazaji wa Injili ya Furaha unaohimizwa na Baba Mtakatifu
Francisko kama sehemu ya ushiriki wa azma ya Uinjilishaji Mpya. Huu ni ushuhuda wa
imani tendaji unaojionesha katika uhalisia wa maisha ya waamini kila siku nchini Korea
ya Kusini. Majadiliano ya kidini na kiekumene ni nyenzo msingi hata katika kuimarisha
umoja na mshikamano wa kitaifa.
Karne ya ishirini imeacha madonda na mahangaiko
makubwa kwa wanachi wa Korea kutokana na vita iliyopelekea mgawanyiko wa Korea mbili
bila kusahau majanga yaliyosabishwa na vita hii, ambayo kamwe haitasahaulika miongoni
mwa wananchi wa Korea, kwani hadi leo hii kuna hatari kwamba, Nchi hizi mbili ambazo
kimsingi ni pacha zinaweza siku moja kupimana nguvu kwa njia ya mtutu wa bunduki.
Katika kipindi chote hiki, Wakristo na Waamini wa dini mbali mbali nchini
humo kwa njia ya majadiliano ya kiekumene na kidini wamejitahidi kupandikiza mbegu
ya msingi wa haki, amani; kwa kukazia haki msingi za binadamu. Tangu mwaka 1924 hadi
leo hii, Korea imepiga hatua kubwa katika mchakato wa majadiliano ya kiekumene.
Wataalam
wa majadiliano ya kiekumene wanasema, kuna haja kwa Makanisa kuendelea kuwekeza katika
majiundo makini ya kiekumene, ili Wakristo kwa pamoja waweze kutolea ushuhuda wao
amini kwa Kristo na Kanisa lake. Waamini hawana budu kuachana na falsafa ya kutumia
nguvu na badala yake waunganishe nguvu zao katika kujenga na kudumisha misingi ya
haki, amani, upatanisho na utulivu.