Kanisa linapenda kukazia majadiliano yanayojikita katika ukweli, uwazi na heshima!
Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican anasema Kanisa Katoliki nchini China
liko hai na linazidi kuchapa kazi, kwa kuendelea kuwa aminifu kwa Injili ya Kristo,
licha ya magumu na changamoto mbali mbali linalokabiliana nazo.
Kardinali
Parolin katika mahojiano maalum na Jarida la "Famiglia Cristiana" linalochapishwa
nchini Italia anasema, Vatican inapenda kukazia majadiliano yanayojikita katika: ukweli,
uwazi na heshima na viongozi wa Serikali ili kupata muafaka wa changamoto na vikwazo
vinavyopelekea waamini wa Kanisa Katoliki kunyimwa uhuru wa kuabudu. Lengo la majadiliano
haya ni kuhakikisha kwamba, kunakuwepo na mazingira mazuri ya uhuru wa kidini.
Kardinali
Parolin akizungumzia hija ya kitume ya Baba Mtakatifu Francisko nchini Korea ya kusini
inayoanza rasmi tarehe 13 hadi tarehe 18 Agosti 2014, ili kushiriki katika maadhimisho
ya Siku ya Sita ya Vijana Barani Asia, inayoongozwa na kauli mbiu "Ondoka, uangaze,
kwa kuwa nuru yako imekuja, na utukufu wa Bwana umekuzukia" anasema kwamba, utafiti
uliofanywa hivi karibuni nchini Korea ya Kusini unaonesha kwamba, Kanisa Katoliki
linaendelea kutoa mchango mkubwa katika maisha na maendeleo ya watu: kiroho na kimwili.
Baba
Mtakatifu anakwenda nchini Korea kama mjumbe wa haki, amani na upatanisho, kwa kutoa
changamoto kwa Korea zote mbili kuweka tofauti zao za kisiasa zilizopelekea chuki
na uhasama kwa kuanza kujikita katika mchakato wa upatanisho wa kitaifa, ili kujenga
umoja na mshikamano kati ya wananchi wa Korea hizi mbili.
Ni matumaini ya Kardinali
Pietro Parolin kwamba, ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko utaweza kukuta mioyo na
akili ambazo zitaupokea na kuufanyia kazi, kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wananchi
wa Korea zote mbili. Korea ya Kusini imebahatika kuwa ni nchi ya kwanza Barani Asia
kuonesha ukarimu kwa kumpokea Baba Mtakatifu Francisko, hapa inaonesha jinsi ambavyo
Baba Mtakatifu anajali na kuguswa na mchango unaotolewa na Kanisa mahalia.