Ongezeko la uzalishaji na matumizi ya umeme linaweza kukoleza maendeleo Barani Afrika
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amesema
kuwa moja ya sababu kubwa zinazokwamisha maendeleo makubwa zaidi na ya haraka zaidi
ya Afrika ni uzalishaji mdogo na matumizi ya chini mno ya umeme. Aidha, Rais Kikwete
amesema kuwa hali hiyo inaeleza jinsi ongezeko la uzalishaji na matumizi ya umeme
linavyoweza kuharakisha maendeleo ya Afrika na kuleta manufaa ya dhahiri kwa kila
familia na kwa kila Mwafrika.
Rais Kikwete ameyasema hayo Jumatano, Agosti
6, 2014, wakati alipozungumza kwenye Mkutano wa Kwanza wa Wakuu wa Nchi za Bara la
Afrika uliofanyika chini ya uenyekiti wa Rais Barack Obama, ambaye ni mwenyeji wa
Mkutano huo. Rais Kikwete amewaambia wakuu wa nchi hizo kwenye Ukumbi wa Mikutano
wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani kuwa ni dhahiri kuwa bila ongezeko kubwa la
uzalishaji na matumizi ya umeme Bara la Afrika halitatoka kwenye uduni.
Rais
amesema kuwa kwa mujibu wa Ripoti ya Kanda ya Shirika la Umoja wa Mataifa Mazingira
(UNEP) “Efficient Lighting in Sub Saharan African Countries” matumizi ya umeme katika
Bara zima la Afrika ni asilimia 31 tu na hivyo kulifanya Bara la Afrika kutumia asilimia
tatu tu ya umeme wote duniani. Rais Kikwete amesema kuwa ili kuelewa udogo wa matumizi
ya umeme ya Bara la Afrika ni kuangalia matumizi ya nishani hiyo kwa kila mkazi wa
Bara hilo na yule wa Marekani. Amesema kuwa wakati kila raia wa Marekani anatumia
kilowati 13, 246 katika Afrika wastani ni kilowati 440.
Ameongeza Rais Kikwete:
“Ukiondoa Afrika Kusini, matumizi ya umeme kwa kila raia wa Afrika yanateremka na
kufikia kilowati 160 tu.” Amefafanua Rais Kikwete: “Uzalishaji wa jumla wa umeme wa
Bara la Afrika ni gigawati 63 ambazo ni sawa na umeme unaozalishwa na nchi moja tu
ya Ulaya – Hispania. Ukiondoa Afrika Kusini, nchi zinazobakia wa Afrika zina uwezo
wa kuzalisha gigawati 28 tu, kiasi ambacho kinazalishwa na nchi moja tu ya Marekani
Kusini ya Argentina.”
Rais Kikwete ambaye alikuwa anafafanua jinsi utoaji huduma
ulio dhahiri unavyoweza kunufaisha wananchi na kujenga mazingira ya taasisi zisizokuwa
za kiserikali kushamiri, ametaja mambo mengine ya msingi ambayo ni lazima yawepo ili
wananchi waweze kunufaika ikiwemo elimu, ushamiri wa sekta binafsi, sera sahihi za
kiuchumi, uwekezaji katika ujenzi wa miundombinu na uboreshaji wa kilimo.
Pia
Rais Kikwete ametaja mambo mengine muhimu yanayoweza kusaidia kuboresha maisha ya
wananchi kuwa ni uendelezaji na matumizi ya teknolojia ya habari na mawasiliano pamoja
na kulea na kukuza demokrasia, utawala bora na utawala wa sheria.