2014-08-08 11:02:31

Hiroshima na Nagasaki, iwe ni fundisho kwa Jumuiya ya Kimataifa!


Baraza la Makanisa Ulimwenguni linasema kwamba, imekwishayoyoma takribani miaka sabini tangu Jumuiya ya Kimataifa iliposhuhudia Hiroshima ikilipuliwa kwa bomu la Atomik hapo tarehe 6 Agosti na mji wa Nagasaki, ukawaka moto hapo tarehe 9 Agosti 1945.

Haya ni matukio ambayo Jumuiya ya Kimataifa inapaswa kuyakumbuka ili yasijirudie tena, kwani yamekuwa ni chanzo cha mateso na mahangaiko ya watu wengi wasiokuwa na hatia hadi leo hii. Wahanga wa vita hii wanaendelea kuililia Jumuiya ya Kimataifa kutorudia tena kwa kosa hili. Lakini, jambo la kusikitisha ni kuona kwamba, hata leo hii bado kuna nchi ambazo zinajihusisha na kutengeneza, kulimbikiza pamoja na kufanya majaribio ya silaha za kinyuklia.

Baraza la Makanisa Ulimwenguni katika mkutano wa Kamati kuu ya Baraza la Makanisa Ulimwenguni, uliowajumuisha wajumbe 150 linasema kwamba, uwepo wa silaha za kinyuklia unakinzana kabisa na dhana ya amani duniani. Silaha za kinyuklia hazina budi kuondolewa katika uso wa dunia, ili kweli amani na utulivu viweze kutawala.

Utengenezaji wa nishati ya kinyuklia ni kielelezo cha matumizi mabaya ya kazi ya uumbaji. Hiroshima na Nagasaki, liwe ni fundisho kwa Jumuiya ya Kimataifa kusitisha utengenezaji, ulimbikizaji na matumizi ya silaha na nishati ya kinyuklia, kwani maafa yake ni makubwa kwa umma wa binadamu na mazingira yake.







All the contents on this site are copyrighted ©.