2014-08-07 15:05:41

Tafakari ya Neno la Mungu, Jumapili ya 19 ya Kipindi cha Mwaka A wa Kanisa


Mpendwa msikilizaji wa Neno la Mungu, leo tunatafakari pamoja masomo Dominika ya 19 ya mwaka A wa Kanisa. Tunaalikwa kugundua sura ya Mungu katika Kristo mfufuka ambaye anatuonesha uwezo na nguvu ya Mungu Baba katika upole na unyenyekevu. RealAudioMP3

Tukiongozwa na Nabii Eliya tunamwona Mungu aliye mnyenyekevu. Hata hivyo ili nabii afikie hapo kwanza anaonekana kuwa mtu aliyekata tamaa baada ya kazi yake ya unabii kuonekana kutozaa matunda mapema. Yuko katikati ya Waisraeli ambao wamemwacha Mungu na kuchukua tamaduni za kipagani. Anatarajia Mungu awaadhibu hawa kwa nguvu lakini Mungu hatendi hilo.

Mawazo haya yanajionesha katika nabii pale mlimani Horeb anapotarajia Mungu ajioneshe katika alama ya upepo wa nguvu, ngurumo na moto mkali, lakini badala yake Mungu anajionesha katika upepo mtulivu na mwanana! Anajifunua kwa nabii Eliya ili atoke katika mtizamo wa kipagani na kuingia katika mapenzi ya Mungu.

Mpendwa sisi tuna picha gani juu ya Mungu? Wakati fulani naona tunayo picha ya Mungu apatilizaye wadhambi wote. Zaidi wakati fulani tuko kama Wana wa Israeli ambao walimkataa Masiya kwa sababu hakuja kwa mabavu badala yake alikuja amepanda mwanapunda! Walitaraji awaondoe katika utawala wa kirumi kwa nguvu za kivita lakini hakuwa hivyo na matokeo yake walimkataa na kumwua! Kwa sababu hiyo Mtume Paulo anawasikitikia Waisraeli, anashangaa kwa nini hawaoni zawadi hiyo kubwa ya kuja kwa mkombozi katikati yao! Mpendwa kuweni macho ili mshangao wa Mtakatifu Paulo usikupate!

Mwinjili Matayo anatusaidia kuelewa Mungu wetu ni yupi. Anasema ni yule ambaye anasali pale mlimani, anayewaponya wagonjwa, anayewalisha wenye njaa. Zaidi Mungu ni nguvu dhidi ya mwovu shetani. Jambo hili linajionesha pale Kristo anapotembea juu ya bahari. Kwa watu wa kale bahari ni kielelezo cha shetani na hivi kutembea juu ya bahari ni kumkanyaga shetani na nguvu zake. Kumbe Kristu ni ushindi dhidi ya vitisho vyote vya shetani.

Kristu aliye upendo haachi Kanisa lake bila nguvu hiyo, kumbe anawakabidhi mitume nguvu hiyo ili wakanyage maovu wanaposimamia taifa lake. Jambo hili liko wazi pale Kristo anapomwambia Mtakatifu Petro atembee juu ya bahari. Hata hivyo haachi kuwaambia kuwa ikiwa imani itapungua mtazama kama Mtakatifu Petro anavyozama, lakini mkiomba msaada wangu nitawaokoa na ndivyo mara moja Mtakatifu Petro anaomba msaada wa Mungu na kuokolewa.

Mpendwa, katika maisha yako umepewa nguvu ya kumkanyaga shetani kwa ubatizo, yafaa kuitumia daima nguvu hiyo kubaki katika upendo wa Mungu na kuepuka kuzama katika ulimwengu kasi unaokuza ubinafsi na utamaduni wa kujipenda zaidi, utamaduni uelekeao katika kifo.

Kwa tafakari hii tunaalikwa kutambua kuwa Mapenzi ya Mungu ni tofauti na mapenzi yetu, Mungu wetu ni mfufuka, ni mshindi dhidi ya dhambi, mwenye huruma kwa wote. Tumsifu Yesu Kristo. Tafakari hii imeletwa kwenu na Padre Richard Tiganya, C.PP.S.








All the contents on this site are copyrighted ©.