Shule kuu ya Sheria, Chuo kikuu cha SAUT, Tanzania
Dr. Adelardus Kilangi, Mkuu wa Shule kuu ya Sheria, Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agostino
cha Tanzania, SAUT katika mahojiano maalum na Radio Vatican anagusia historia fupi
ya Shule kuu ya Sheria na tofauti iliyopo kati ya Shule kuu ya Sheria na Kitivo cha
Sheria. Anasema, Shule kuu ya Sheria inakazia zaidi vitendo, kwa kuwasaidia wanafunzi
kujifunza kwa vitendo, kuzungumza na kujenga hoja.
Shule kuu
ya Sheria, Chuo Kikuu cha SAUT imeonesha mafanikio makubwa nchini Tanzania kwa wanafunzi
kutoka SAUT wana soko kubwa la fursa ya ajira, kwani ni wanafunzi waliofundwa wakafundika,
tayari kukabiliana na changamoto katika uwanja wa sheria. Shule kuu ya Sheria imeonesha
mafanikio makubwa pia Afrika Mashariki na kwamba, inaendelea kufanya vyema katika
taaluma na tafiti mbali mbali, mambo msingi katika kuwajengea wanafunzi uwezo katika
masuala ya sheria.
Dr. Adelardus Kilangi anasema kwa wanafunzi wanaotaka kujiunga
na Shule ya sheria wanakaribishwa kwa mikono miwili, lakini watapaswa kuzingatia viwango,
uwezo na kufanya kazi kwa juhudi na maarifa. Ni watu wanaotakiwa kusoma kwa ari kuu,
ili waweze kubobema katika taaluma, kwa kuzingatia: kanuni maadili na viwango.
Dr.
Adelardus Kilangi anawahimiza wadau mbali mbali katika mfumo wa sheria na wananchi
wote kwa ujumla kuendeleza utawala wa sheria, kwa kuzingatia haki msingi za binadamu,
ili kukuza kudumisha amani, upendo na mshikamano kati ya watu, kwani bila haki, amani
na utulivu, maendeleo ya mwanadamu yako mashakani!