Mshikamano wa Papa Francisko kwa Wakristo huko Iraq!
Baba Mtakatifu Francisko anafuatilia kwa umakini na wasi wasi mkuu hali ya Wakristo
huko Mashariki ya Kati, kutokana na habari za kutisha zinazoendelea kutolewa na watu
mbali mbali hususan Kaskazini mwa Iraq. Waathirika wakuu ni Wakristo ambao wamelazimika
kuyakimbia makazi yao kutokana na vita inayoendelea huko Iraq.
Wakristo wanateswa
na kudhulumiwa, kiasi cha kulazimika kukimbia bila hata ya kuchukua mahitaji msingi.
Baba Mtakatifu wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana, Jumapili tarehe 20 Julai 2014 alipenda
kuonesha mshikamano wake wa dhati na Wakristo huko Iraq. Baba Mtakatifu anapenda kuwahikishia
uwepo wake katika imani kwa Kristo aliyeshinda dhambi na mauti!
Baba Mtakatifu
anaendelea kuungana na viongozi wa kidini na watu wote wenye mapenzi mema, ili kuendelea
kumwomba Roho Mtakatifu ili awasaidie kupata zawadi ya amani. Baba Mtakatifu anaiomba
Jumuiya ya Kimataifa, kusaidia mchakato wa kusitisha vita na madhulumu dhidi ya Wakristo;
kwa kuwasaidia wakimbizi na wahamiaji wanaotafuta hifadhi katika maisha yao. Hili
ni kundi la watu ambalo linahitaji mshikamano wa upendo.
Baba Mtakatifu anasema
Padre Federico Lombardi anawaombea watu wote, ili Mwenyezi Mungu, kisima cha amani
aweze kuamsha ndani ya watu kiu ya kutaka kuanzisha mchakato wa majadiliano na upatanisho.
Baba Mtakatifu anasema, ubaya hauwezi kushindwa kwa njia ya ubaya. Vita inashindwa
kwa njia ya amani.