2014-08-07 15:44:38

Ebo! Eti Petro anataka kufanya Sarakasi juu ya Bahari!


Ili tuweze kuelewa sawasa ujumbe wa Injili ya leo, huna budi kukumbuka maelezo ya wiki iliyopita juu ya muujiza wa mikate na mapendekezo anayotoa Yesu. Mara baada ya hapo “Yesu akawalazimisha wanafunzi wake wapande chomboni na kutangulia mbele yake kwenda ng’ambo, wakati yeye alipokuwa akiwaaga makutano.”

Yesu anawalazimisha wanafunzi kutoka nchi ya uyahudi na kuvuka ng’ambo kwenda nchi ya upagani. Yaonekana wanafunzi wenyewe hawakupenda kwenda. Budi tuelewe kwamba, masimulizi ya Injili siyo mfululizo wa matukio ya kihistoria ya kufuatika kimantiki (chronic).

Mfano, Yesu anawalazimisha wanafunzi waende peke yao chomboni usiku kama wanavyoshuhudia wanafunzi wenyewe pale walipomtaka Yesu awaache watu waende vijijini kununua chakula. Aidha baada ya kugawa mikate kwa watu elfu tano, muda ulishapita sana. Yasemwa pia kwamba chombo kilichukua muda mrefu sana kuvuka, ingawaje ziwa lilikuwa dogo tu. Halafu haieleweki ni kwa nini Yesu anawaacha wanafunzi wahangaike ziwani peke yao pindi mwenyewe anajiendea mlimani usiku peke yake kusali. Kadhalika unamwona Petro aliye fundi wa kuogelea (mvuvi) anaogopa na anataka kuzama. Matukio haya yote ni maelezo ya kitaalilimungu.

Mazingira ni kwamba wanafunzi walikuwa wanatoka kulishwa Neno lenye uwezo wa kutenda muujiza wa kuumba ulimwengu mpya. Kwa miaka mitatu Yesu analitangaza Neno hilo katika uyahudi tu. Sasa ni kazi ya mitume kulipelekea Neno hilo kwa watu wote ulimwenguni. Tunaona vikapu kumi na viwili vilivyojaa, yaani kila mtume anakuwa na kikapu kimoja.

Kwa hiyo, Mitume wameitwa kuwa Wamisionari wa kupeleka chakula hiki (Neno) ulimwenguni kote. Chombo (mashua) ambacho Yesu Kristu anawalazimisha wanafunzi kusafiria ni Jumuia ya kikristo, yaani Kanisa. Yesu anawaaga makutano kisha anapanda mlimani kuomba. Hapa halitajwi jina la mlima na katika lugha ya kibiblia mlima unamaanisha ulimwengu wa Mungu.

Kwa hiyo Yesu anaingia katika ulimwengu wa Baba yake. Wakati ni jioni: “Kulipokuwa jioni alikuwako huko peke yake.” Majira hayo katika Biblia yana maana hasi. Yaani Yesu angekuwa pamoja nao giza lisingekuwepo, hali ingekuwa angavu, na ya kuleta matumaini. Bila Yesu kila kitu ni usiku wa giza bila matumaini. Aidha, jioni ni lugha ya fumbo yenye maana ya mwisho wa maisha ya Yesu, yaani mwisho wa uwepo wake kimwili duniani. Anatoweka na kuingia katika ulimwengu wa Baba (kupaa mbinguni). Wanafunzi wanajisikia pweke, gizani na wanakosa matumaini wanakosa mwelekeo wa maisha.

Wakati huo ndiyo “Chombo kimekwisha kufika katikati ya bahari, kinataabika sana mawimbi.” Maji ya bahari, mawimbi na dhoruba ni alama ya nguvu za kifo kama ilivyokuwa gharika kuu, au katika maji ya bahari ya shamu yaliyowazamisha wamisri nk. Maji yanaogopesha sana. Kwa watu wa pwani walioathiriwa na fikra za watu wa mashariki ya mbali, wanaogopa maji wakiamini kwamba bahari hukaa viumbe vya kudhuru viitwavyo “majini.”

Kutaabika kwa Chombo kwamaanisha kupambana na upepo wa mbisho, unaoenda kinyume cha kinakokwenda chombo kupeleka ujumbe Neno la Kristu. Upepo wa ulimwengu huu ni ule unaotaka kuendeleza hali ya ulimwengu wa zamani. Imani kishirikina zinazoogopesha ndiyo hayo majini yanayobeba picha ya madhulumu, madharau, kebehi, kuchukiana, nk.

“Hata wakati wa zamu ya nne ya usiku Yesu akawaendea, akienda kwa miguu juu ya bahari.” Ni asubuhi yaani, mwanzo wa siku. Wanafunzi wanapomwona anatembea juu ya bahari, wanafadhaika na kusema, “Ni kivuli (jini) wakapiga yowe kwa hofu.” Kwa bahati wanafunzi wanafahamu kwamba ni Mungu peke yake ndiye anayeweza kutembea juu ya maji. Katika kitabu cha Job kuna fasuli inayosema: “Mungu peke yake ndiye mwenye uwezo wa kutembea juu ya mawimbi ya maji, na ni Mungu peke yake aliweza kugawa bahari ya shamu.

Ni Mungu peke yake anayeweza kutawala maji ya bahari na kila kitu kilichomo kinachopingana na maisha.” Lakini hapa wanafunzi hawakumtambua bado Yesu kuwa ni Emmanueli, yaani Mungu nasi. Hii ndiyo jumuia inayosafiri katika mawimbi ya bahari, inafadhaika na inashindwa kujua ni kitu gani hasa kinachotembea juu ya bahari. Ndiyo maana wanakipachika jina linaloonesha woga mkubwa walio nao wanakiita: “Kivuli” na wanagumia kwa hofu.

Yesu anawatuliza: “Jipeni moyo, ni mimi, msiogope.” Hii ni lugha ya kiteolojia, ambayo Mateo anaitumia akichanganya na lugha ya kibiblia katika mazingira ya jumuia ya wakristu wa kwanza waliokuwa wanapambana na misukomisuko mingi. Wakristu hao hawakuwa tena na Yesu kimwili, hivi hawakujiamini, hawakujisikia usalama, hawakuwa na nguvu, walikuwa karibu kukata tamaa. Kumbe Yesu alikuwa nao daima kama “Kivuli”.

Lugha hii inafanana na ile ya Injili ya Luka baada ya ufufuko wa Yesu, ambapo “mitume walishituka, wakaogopa sana, wakidhani ya kwamba wanaona roho” (Lk 24:37). Ingawaje picha hii ya Yesu mfufuka ni finyu lakini inabaki kuwa ndiyo namna ya kumweleza Yesu mfufuka kuwa yu pamoja nao kwa namna tofauti na ilivyokuwa mwanzoni.


Mashaka aina hii ya wakristu wa kwanza tunaweza kuwa nayo hata sisi leo tunapopambana na matatizo ya kujenga ulimwengu alioutangaza Bwana. Tunafadhaika mbele ya upepo mwingi wa mbisho unaotutisha na tunamtafuta Yesu wa Nazareti anayeweza kushikika, kumbe yeye anaonekana kama “kivuli” au “roho”, picha finyu ioneshayo hali mpya ya Yesu mfufuka. Kumbe tusimtafute Yesu anayeshikika.

Katika majadiliano kati ya Petro na Yesu yanajitokeza maombi mawili ya Petro kwa Yesu. Ombi moja ni zuri na lenye faida kwetu. Ombi la pili halina maana. Petro anasema: “Bwana, ikiwa ni wewe, niamuru nije kwako juu ya maji.” Yesu akasema: “Njoo”. Ombi la kwanza, anaomba kumwendea Yesu. Hapa yaonekana Petro amemtafakari Yesu mfufuka aliyeishavuka bahari ya mauti na yuko katika ulimwengu wa Mungu. Aidha Petro anajua kuwa ameitwa kufuata mapendekezo ya Kristo na anataka kumfuata. Ombi hili la kumwendea na la kukutana Yesu limekaa vizuri.

Kwamba, sote tulioitwa kwa ubatizo kumfuata Yesu, tuwanie daima kumwendea na kukutana naye katika maisha yetu. Ombi la pili Petro anataka kutembea juu ya maji. Yaani, Petro anataka kumwendea Yesu kwa kufanya matendo ya kimaajabu (sarakasi) ya kutembea juu ya maji.

Mapato yake badala ya kumwangalia Yesu, anaangalia jinsi anavyoweza kutembea juu ya maji wakati wa dhoruba kali. Mapato yake Petro anaponzeka, anapata wasiwasi na kutaka kuzama. Huu ndiyo mtego mkubwa unaowaponza watangazaji wengi wa Injili. Yaani kuzingatia zaidi maajabu anayoweza kuyatenda kuliko kumtazama kristu.

Fundisho kuu ni kwamba tutaonana na Yesu siyo katika kufanya miujiza na mambo ya pekee, bali katika matendo ya kawaida ya kila siku. Mapendekezo aliyotoa Yesu ni yale ya kutofuata mambo ya ulimwengu huu bali kujenga ulimwengu wa upendo. Ili kufanya hivyo yabidi kuacha maisha yako na kujitolea wewe mwenyewe kwa ajili ya ndugu hicho ndicho kifo kinachotisha.

Kutisha huko kutaisha pale Petro anapofaulu kukaza macho yake kumwelekea Yesu. Hapo anapata tena nguvu na kufanikiwa kumwendea, lakini pale imani yake inapotetereka na kusita katika kujitoa maisha yake kwa ajili ya ndugu, pale anapowaza juu ya kifo na juu ya kupoteza maisha, hapo anaanza kuzama.


Tunaalikwa kumwangalia na kumwiga alichofanya, alichopitia Yesu, nasi tutakuwa na nguvu ya kumfuata. Tukiwa na mashaka tutaanza kuzama kisha tutaingiwa na woga na kupiga mayowe. Leo Yesu anatupatia ushauri wa bure: “Mkiniaminia na kulifuata Neno langu, maji na mawimbi ya maji ya kifo hayatawatisha kamwe. Mtavuka tu mkiwa ndani ya mashua (kanisa) hata kama kuna mawimbi na dhoruba kali na mtanikuta katika ufufuko.”

Padre Alcuin Nyirenda, OSB.








All the contents on this site are copyrighted ©.