2014-08-07 10:39:30

CUEA na mikakati ya kuwajengea viongozi wa AMECEA uwezo katika shughuli za kichungaji!


Monsinyo Pius Rutechura, Makamu mkuu wa Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha Afrika Mashariki, CUEA, kilichoko Nairobi, Kenya, katika mahojiano maalum na Radio Vatican anabainisha misingi ya mikuu ya CUEA katika kuwajengea uwezo viongozi wa Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika Mashariki na Kati, AMECEA katika mikakati na shughuli zao za kichungaji. RealAudioMP3

Hii ni programu inayoendeshwa kwa ushirikiano kati ya CUEA na Baraza la Maaskofu Katoliki Marekani. Lengo ni kutaka CUEA iweze kuimarisha huduma kwa Familia ya Mungu katika Nchi za AMECEA, ili kushiriki kikamilifu katika mchakato wa Uinjilishaji mpya, utume unaovaliwa njuga na Mama Kanisa katika mapambazuko ya Millenia ya tatu ya Ukristo.

Monsinyo Rutechura anasema kwamba, Vyuo vikuu vya Kikatoliki havina budi kuzingatia mtazamo, vipeo na utume wake ndani na nje ya Kanisa. Haya ni mambo msingi yanayopaswa kuongoza ushindani unaofanywa katika sekta ya elimu ya juu. Ikumbukwe kwamba, vyuo vikuu na taasisi za elimu ya juu zinazomilikiwa na kuendeshwa na Mama Kanisa ni vyombo vya Uinjilishaji makini vinavyopaswa kuzingatia kanuni maadili, Mapokeo na Mafundisho ya Kanisa Katoliki, kwa kumwangalia mtu mzima: kiroho na kimwili.

Monsinyo Rutechura anasema, hii ni elimu inayojikita katika kumjengea mwanafunzi maadili mema, uwezo wa kuwajibika kwa kuheshimu: hadhi, utu na heshima ya binadamu. Hii ni elimu inayotafuta ukweli mkamilifu kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa uwepo wa Mungu katika maisha na vipaumbele vya mwanadamu. Licha ya maendeleo ya sayansi na teknolojia, lakini mwanadamu bado anahitaji sayansi na elimu itokayo juu.

Monsinyo Pius Rutechura anasema Kanisa lina hazina kubwa katika sekta ya elimu, mambo yanayojionesha katika Nyaraka mbali mbali, kumbe ni wajibu wa wadau wa sekta ya elimu katika Kanisa kufanya rejea katika nyaraka hizi, ili ziweze kuwasaidia katika mchakato wa utoaji wa elimu ya juu kadiri ya mafundisho ya Kanisa Katoliki pamoja na kuendelea kusoma alama za nyakati.







All the contents on this site are copyrighted ©.