2014-08-06 10:49:26

Ugonjwa wa Ebola unatisha!


Jumuiya ya Kimataifa inaendelea kuonesha ushirikiano mkubwa katika mapambano dhidi ya ugonjwa wa Ebola ambao kwa sasa umekuwa ni tishio la usalama na maisha ya wananchi wengi, Kaskazini Magharibi mwa Afrika. Rais wa Benki ya Dunia Bwana Jim Yong Kim anasema, Benki ya Dunia imetoa kiasi cha dolla za kimarekani millioni mia mbili, ili kusaidia mapambano dhidi ya ugonjwa wa Ebola.

Tamko hili limetolewa wakati wa mkutano kati ya Marekani na Wakuu wa Nchi za Afrika ambao wako mjini Washington DC. kujadiliana kuhusu ushirikiano kati ya Marekani na nchi za Kiafrika. Fedha hii inalenga kudhibiti ugonjwa wa Ebola nchini Guinea, Sierra Leone na Liberia. Shirika la Fedha la Kimataifa, IMF, linasema kwamba, kutokana na kuzuka kwa ugonjwa wa Ebola, uchumi wa Guinea unaweza kuyumba kwa kiasi kikubwa.

Shirika la Afya Duniani katika taarifa yake iliyotolewa mapema juma hili, zinaonesha kwamba, hadi sasa kuna watu 887 waliokwishafariki dunia na watu 1, 063 wameambukizwa virusi vya Ebola. Marekani imetuma kikosi cha mabingwa hamsini kwenda katika nchi ambazo kwa sasa zimeathirika kwa ugonjwa wa Ebola, ili kuangalia namna ya kuweza kuudhibiti kwani kwa sasa Ebola ni tishio kwa Jumuiya ya Kimataifa.







All the contents on this site are copyrighted ©.