2014-08-06 09:22:59

Mchakato wa malezi ya miito mitakatifu!


Vijana wa kizazi kipya wanapata taabu sana kusikiliza sauti ya Mungu inayowaita kujitosa kimasomaso kwa ajili ya kumtumikia Yeye na Jirani zao, kwa njia ya miito mitakatifu ndani ya Kanisa. Ni vijana ambao wametekwa na makelele mengi kiasi kwamba inakuwa vigumu kuweza kupambanua sauti ya Mungu na makelele yanayowazunguka, kwani wakati mwingine wanakumbana na utupu katika maisha yao ya ujana. RealAudioMP3

Kumbe, jambo la msingi ni kuwasaidia vijana hawa kuona ile njia ya imani, kwa kuwasikiliza kwa makini na kuwaongoza pole pole katika hali ya ukimya, kwani Mungu daima anazungumza na watu wake kwa njia ya ukimya, katika undani wa maisha ya mwanadamu.

Hii ni changamoto ambayo imetolewa na wajumbe waliokuwa wanahudhuria mkutano wa kimataifa ulioandaliwa na Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Barani Ulaya kuhusu miito. Wajumbe wameshirikisha uzoefu na mang’amuzi yao katika kuwasindikiza vijana kusikiliza na hatimaye, kuitambua sauti ya Mungu inayowaalika kujisadaka kwa ajili ya Mungu na Kanisa lake.

Kongamano hili limefanyika hivi karibuni Jimboni Varsavia, Poland. Kongamano la miito kwa mwaka 2015 litaanza kushika kasi hapo tarehe 6 hadi 9 Julai 2015 na litafanyika mjini Prague. Kauli mbiu ya kongamano la mwaka huu ilikuwa ni “Elimu inayojikita kwa Yesu kwa ajili ya huduma kwa miito nyakati hizi”.

Ni kongamano ambalo limewashirikisha wakurugenzi wa miito na wadau mbali mbali wanaojihusisha katika kuwasaidia vijana kusikia sauti ya Mungu inayowaalika kujisadaka kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake. Wajumbe wameonesha wasi wasi wao kutokana na kuendelea kupungua kwa miito ya maisha ya Kipadre na Kitawa Barani Ulaya. Ushiriki wa waamini katika maisha na utume wa Kanisa unaendelea kufifia mwaka hadi mwaka.

Hapa wajumbe wanasema, kuna haja ya kushiriki kikamilifu katika mchakato wa Uinjilishaji mpya kwa njia ya ushuhuda wa maisha unaodhihirisha imani tendaji katika uhalisia wa maisha. Vijana wafundishwe kujenga na kudumisha utamaduni wa watu kukutana kama anavyokazia Baba Mtakatifu Francisko katika maisha na utume wa Kanisa. Ushuhuda wa imani tendaji ni kati ya mambo ambayo yanaweza kuleta mvuto na mashiko kwa vijana kuweza kusikia na hatimaye, kujisadaka kwa ajili ya Mungu na jirani. Hapa Kristo anapaswa kupewa kipaumbele cha kwanza katika maisha na utume wa Kanisa.

Uinjilishaji mpya ndiyo dhana inayopaswa kufanyiwa kazi kwa sasa badala ya kuendekeza mtindo wa maisha wa zamani, ili kuwapatia vijana fursa ya kutambua na kuonja upendo wa Mungu katika maisha, ili hatimaye, kufanya maamuzi magumu na endelevu, kwa ajili ya kujisadaka, ili kushiriki katika maisha na utume wa Kanisa.

Haya ni maisha yanayoonesha shukrani kwa Mwenyezi Mungu kwa zawadi ya Upadre na Utawa. Vijana waelimishwe na kuelekezwa umuhimu wa kujikita katika hija ya utakatifu wa maisha, kwa kukutana daima na Yesu Kristo kwa njia ya Sala, Tafakari, Sakramenti na Matendo ya huruma.

Imehaririwa na
Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.







All the contents on this site are copyrighted ©.