2014-08-06 10:00:53

Kuweni mwanga na chumvi ya Dunia Papa awaasa vijana


Baba Mtakatifu Francisko Jumanne jioni, alikutana na watumishi wa altareni, wapatao 50,000 kutoka Ujerumani na nchi jirani ya Uswiss na Austria. Vijana hao, wenye umri kati ya miaka 13 -27, kila mwaka huwa na ratiba ya kufanya hija katika Madhabahu Matakatifu yaliyoko jijini Roma na Vatican. Kwa mwaka huu, hija yao imeongozwa na kauli mbiu: "Ni huru sababu ni halali kutenda mema".


Baba Mtakatifu alikutana na vijana hawa katika uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro, walioufanya uwanja huo kuwa hai na sura ujana, ukipambwa zaidi na muziki hai wa kisasa. Papa baada ya kuwazungukia vijana akiwa katika gari lake la Kipapa, aliwasalimia na kufurahi pamoja nao . Na kisha aliongoza Ibada ya Masifu ya Jioni , na kuwahutubia kwa lugha ya kijerumani, ambamo hotuba yake ililenga katika kufafanua somo kutoka waraka kwa Wagalatia, maneno ya Mtakatifu Paulo “ punde tu tumesikia ... kuvutia mawazo yetu. Wakati umetimia”.

Papa Francisco alifafanua maneno: sasa ni wakati, Wakati Mungu amekamilisha kazi yake. na kufafanua kuwa maneno haya yanatuonyesha sisi kwamba, Yeye ni Baba Mwema, kupitia Umwilisho wa Mwana, ambaye anakuwa mmoja wetu. Kwa ufahamu huu wa mtu halisi katika jina la Yesu, tunaweza kuelewa nini maana ya Mungu kweli. Yeye anataka kumweka huru binadamu , ili kwamba daima aweze kujisikia salama kama mtoto wa Baba Mwema.


Lakini, Papa alisema,” kuufanikisha mpango huu, Mungu alihitaji mtu binadamu, mwanamke , Mama kumleta Mwanae duniani. Na mwanamke huyo ndiye Bikira Maria, ambaye tunamheshimu katika Ibada hii”. Papa Francisco aliendelea kueleza kwamba , Maria alikuwa huru kabisa.Na katika uhuru wake alichagua kusema" ndiyo" kwa mpango wa Mungu, alisema ndiyo katika kutenda mema. Na hivyo ndivyo yeye alivyochagua kumtumikia Mungu. Alimtumikia Mungu na binadamu.
Kwa maelezo hayo Papa aliwahimiza watu wote kuiga mfano wa Bikira Maria, kama wanataka kujua kile Mungu anatarajia kutoka kwao kama watoto wake.

Baada ya Ibada hii ya Kiliturujia, Papa Francisco , alizungumza na vijana kupitia njia ya maswali na majibu. Alijibu maswali kadhaa kutoka vijana hao watumishi wa altareni. Akijibu moja ya swali alisema dunia, inahitaji watu wa kushuhudia wengine kwamba, Mungu anatupenda, kwamba hakika Yeye ndiye Baba yetu, na vijana wana nafasi ya pekee ya kuwa mashahidi wa hilo katika hija hii ya maisha. Na kwamba Vijana wameitwa na Yesu na wanatakiwa kwa uhuru kabisa kutoa jibu lao, si tu ndani mwao, au parokiani au katika vyama vyao , lakini hasa kwa wale wanaoonekana kuwa mbali na Mungu.


Papa Francisko alionyesha kutambua matatizo ya vijana wengi katika uzoefu wao wa kutunza ahadi yao ya kuendelea kuhudumia Kanisa na shughuli nyingine mbalimbali na kuwatia moyo kwamba, mara nyingi matatizo ni changamoto muhimu katika utamaduni wa makuzi ya binadamu. Na hufundisha mtu kujipanga vyema. Papa aliwasifu vijana hao wa Kijerumani kwamba , wao wanafanya vyema katika hili. Na kwamba kati miongoni mwa mahitaji mengi ya kawaida ya kila siku, Papa alisema, ni muhimu na lazima kutoa vipaumbele kukumbuka kwamba Muumba wetu, ndiye anayetupatia maisha, anatupenda, na huambatana nasi katika hija yetu ya maisha.


Mwisho Papa alirejea Mada ya mwaka huu ya Hija ya Vijana , akisema tumepokea kutoka kwa Mungu zawadi ya uhuru, kwa sababu, tumeumbwa kwa sura na mfano wake. Na kama uhuru huu ukitumiwa vibaya, unaweza kuwa sababu ya kuwa mbali na Mungu, na kutufanya tupoteze hadhi yetu ya kufanana naye aliyotuvalisha sisi. Na ndiyo maana tunahitaji miongozo na sheria, katika jamii na katika kanisa : kutusaidia kufanya mapenzi ya Mungu, na hivyo kuishi kulingana na heshima na hadhi ya kwua watoto wa Mungu.

Baba Mtakatifu aliwasihi vijana wasitumie vibaya uhuru wao ! Wasipoteze hadhi kubwa ya kuwa watoto wa Mungu, waliyopewa bure! Na kama wataandamana na Yesu na Injili yake, uhuru wao, unakuwa kama mmea unaochanua maua na kuzaa matunda mazuri tele! Kwa kutembekea katika njia hiyo ya Yesu, wataweza kutapata furaha halisi, sababu Yeye anataka wawe wanaume na wanawake wenye furaha kamilifu. Ni tu kaika kushikamana na Mapenzi ya Mungu , tunaweza kufanya yaliyo mema na kuwa mwanga na chumvi ya dunia.








All the contents on this site are copyrighted ©.