2014-08-05 08:57:59

Papa Francisko katika mchakato wa mapambano dhidi ya baa la njaa duniani


Shirika la Kilimo na Chakula la Umoja wa Mataifa, FAO, katika taarifa yake kwa vyombo vya habari linasema kwamba, Baba Mtakatifu Francisko anatarajiwa kushiriki katika mkutano wa pili wa kimataifa kuhusu lishe, utakaofanyika kwenye Makao makuu ya FAO mjini Roma, kuanzia tarehe 19 hadi tarehe 21 Novemba 2014. Huu ni mkutano ulioandaliwa kwa ushirikiano kati ya FAO na Shirika la Afya Duniani, WHO. RealAudioMP3

Taarifa hizi zimethibitishwa na Askofu mkuu Luigi Travaglino, Mwakilishi wa kudumu wa Vatican kwenye Mashirika ya Umoja wa Mataifa yaliyoko mjini Roma.

Bwana Josè Graziano da Silva, Mkurugenzi mkuu wa FAO amepongeza hatua ya Baba Mtakatifu Francisko kushiriki katika mkutano wa pili wa lishe, ili kuiwezesha Jumuiya ya Kimataifa kuwa na uhakika a usalama wa chakula. Anasema, gharama ya shughuli za kiuchumi na kijamii zinazidi kuongezeka katika Jumuiya ya Kimataifa, mambo ambayo yanaathiri pia mapambano dhidi ya baa la njaa na utapiamlo duniani, unaoendelea kusababisha majanga makubwa kwa mamillioni ya watu hasa watoto wadogo wanaotoka katika Nchi maskini duniani.

Bwana Graziano da Silva anasema, mkutano wa kwanza ulifanyika kunako mwaka 1992. Mkutano utakaofanyika mwaka huu, unatarajiwa kuhudhuriwa na viongozi wakuu wa Serikali, watunga sera na wawakilishi wa mashirika ya kimataifa na vyama vya kiraia, ili kuangalia kwa pamoja juhudi zilizokwisha fikiwa na Jumuiya ya Kimataifa katika mapambano dhidi ya lishe duni pamoja na kuibua mbinu mkakati wa kuboresha lishe na afya ya watu.

Takwimu zinaonesha kwamba, kuna zaidi ya watu millioni 842 ambao wanakabiliwa na baa la njaa sehemu mbali mbali duniani na kwamba, wengi wao wanapoteza maisha kutokana na baa la njaa au ukosefu wa lishe bora. Watoto millioni 7 wanafariki dunia kabla ya kuadhimisha miaka mitano tangu walipozaliwa; watoto wengine millioni 162 chini ya miaka mitano wamedumaa wakati ambapo kuna watoto millioni 500 wenye unene wa kupindukia.

Taarifa ya FAO inaonesha kwamba, Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa, Bwana Ban Ki-Moon, Rais Giorgio Napolitano wa Italia, Rais Michelle Bachelet wa Chile, Rais Jakaya Mrisho Kikwete wa Tanzania ni kati ya viongozi mashuhuri walioalikwa kwenye mkutano huu.








All the contents on this site are copyrighted ©.