2014-08-05 10:33:57

Mimi na familia yangu tutamtumikia Bwana!


Kongamano la kwanza la Familia kwa ajili ya Nchi za Amerika ya Kusini linaloongozwa na kauli mbiu "Mimi na Familia yangu tutamtumikia Bwana", lililofunguliwa mapema siku ya Jumatatu linatarajiwa kufungwa Jumamosi tarehe 9 Agosti 2014 mjini Panama.

Kongamano hili ni sehemu ya maandalizi ya maadhimisho ya Sinodi maalum ya Maaskofu kwa ajili ya Familia itakayofanyika mjini Vatican kuanzia tarehe 5 hadi tarehe 19 Oktoba 2014.

Kongamano hili limeandaliwa na Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Amerika ya Kusini na Visiwa vya Caribiani. Wajumbe wanaendelea kupembua umuhimu wa familia katika maendeleo ya kijamii sanjari na mshikamano wa kimissionari.

Hapa wajumbe wanaangalia fursa, changamoto na matatizo yanayozikabili familia Amerika ya Kusini katika mchakato wa maendeleo endelevu yanayogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili. Wajumbe wanapenda kutumia fursa hii kwa ajili ya kubainisha sera na mikakati makini inayoweza kusaidia familia kutekeleza nyajibu zake, kwa kusaidiwa na Serikali husika.

Mada nyingine zinazofanyiwa kazi kwa wakati huu ni elimu, mawasiliano, Injili ya uhai, uchumi na mchakato wa Uinjilishaji Mpya unaojikita katika ushuhuda wa maisha adili na matakatifu. Hapa wajumbe wanashirikishana maisha ya kiroho, ili kuibua mkakati wa kichungaji utakaofanyiwa kazi kwa ajili ya kuzijengea uwezo Familia ili ziweze kutekeleza dhamana yake. Kuna sala maalum kwa ajili ya familia na utume wake, ili kuziwezesha familia kutambua na kuendeleza tunu msingi za maisha ya ndoa na familia kadiri ya mpango wa Mungu.

Hapa mambo yanayokaziwa ni tunu msingi za maisha ya kiroho, kijamii na kanuni maadili, ili kujenga ulimwengu unaojikita katika ubinadamu, upendo na mshikamano wa kweli. Ikumbukwe kwamba, Familia ni chemchemi ya uhai, udugu, upendo na amani ya kweli!







All the contents on this site are copyrighted ©.