2014-08-05 10:05:37

Changamoto zinazofanyiwa kazi kati ya Marekani na Viongozi wa Nchi za Kiafrika


Rais Barack Obama wa Marekani kuanzia tarehe 4 Agosti 2014 anafanya mkutano wa siku tatu na viongozi wakuu wa nchi 50 za Kiafrika, ili kuimarisha uhusiano kati ya Marekani na Bara la Afrika. Mkutano huu unafanyika baada ya Rais Obama kutembelea Senegal, Afrika ya Kusini na Tanzania, mwaka 2013. Kwa bahati mbaya mkutano huu unafanyika wakati kuna vita inayoendelea Ukanda wa Ghaza kwa kusababisha vifo na mateso kwa watu wasiokuwa na hatia bila kusahau Ucrain.

Kwa mara ya kwanza mkutano huu ulilenga kuzungumzia masuala ya ushirikiano wa kiuchumi kati ya Amerika na Nchi za Kiafrika. Lakini, tatizo la wahamiaji kutoka Afrika wanaoendelea kufa maji huko kwenye Bahari ya Mediterania; mashambulizi ya kigaidi yanayofanywa na Kikundi cha Boko Haram, vita na kinzani za kijamii zinazoendelea Sudan ya Kusini na Somalia, mlipuko wa ugonjwa wa Ebola; hizi ni kati ya changamoto zinazolikabili Bara la Afrika kwa sasa na bila shaka zitapewa kipaumbele cha pekee katika mkutano huu.

Serikali ya Marekani inataka kuwekeza zaidi katika masuala ya nishati, ili kuwezesha familia millioni ishirini kupata nishati ya umeme, Kusini mwa Jangwa la Sahara. Makampuni ya Marekani yanaendelea kuwekeza kiasi cha dolla za kimarekani billioni tisa katika nishati ya umeme. Haki msingi za binadamu ni kati ya mambo ambayo bado hayajafanyiwa kazi vyema na nchi nyingi Barani Afrika.

Viongozi kutoka Sudan kongwe, Eritrea, Jamhuri ya Watu wa Afrika ya Kati na Zimbabwe hawakualikwa kwenye mkutano huu kati ya Rais Obama na viongozi kutoka Barani Afrika. Marais kutoka Liberia na Siera Leone wamelazimika kufuta ziara hii kutokana na mlipuko wa ugonjwa wa Ebola.







All the contents on this site are copyrighted ©.