Bunge Maalum la Katiba limeanza kutimua vumbi Dodoma!
Hotuba ya Mwenyekiti wa Bunge Maalum la Katiba Mhe. Samuel Sitta katika ufunguzi wa
awamu ya pili ya Bunge hilo, Dodoma tarehe 5 Agosti 2014.
Karibuni tena Dodoma
Waheshimiwa Wajumbe wa Bunge Maalum la kutunga Katiba ya nchi yetu. Sote tuna kila
sababu ya kumshukuru Mwenyezi Mungu wetu kwa kuendelea kutupa uhai na afya hadi leo
kutuwezesha kuwepo ndani ya ukumbi huu. Tupo humu ili tuitekeleze kazi waliyotukabidhi
Watanzania wenzetu milioni arobaini na sita (46) ya kuwapatia Katiba mpya. Dhamana
hii ni nzito na haistahili kufanyiwa ajizi.
Tunaendelea na shughuli zetu za
Bunge Maalum kwa kuzingatia Kanuni ya 30 (1) inayosema "Akidi kwa kila kikao cha
Bunge Maalum isipokuwa wakati wa kupitisha uamuzi wa Bunge Maalum itakuwa ni nusu
ya Wajumbe wote wa Bunge Maalum". Nimetaarifiwa na Katibu kwamba wajumbe waliokuja
Dodoma kuhudhuria ni zaidi ya robo tatu ya Wajumbe wote wa Bunge Maalum. Nawashukuruni
nyote kwa kuja hapa Dodoma ili kutimiza wajibu wenu.
Kwa niaba yenu, nawashukuru
Watanzania wenzetu wote ambao kwa mamilioni wamedhihirisha utashi mwema wa kisiasa
kwa kuunga mkono hatua ya Bunge Maalum kuendelea na kazi zake hadi tuipate Katiba
inayopendekezwa ambayo wataipigia kura ya maoni. Kipekee na kwa niaba yenu, nawashukuru
kwa dhati viongozi wetu wa dini wa madhehebu yote wanaloliombea Taifa hili mafanikio
Bunge Maalum, wakitanguliza utaifa pamoja na amani ya nchi na umoja ndani ya nchi
na siyo ubinafsi na maslahi ya makundi.
Kwa leo sikupenda sana kuzungumzia
hoja mbali mbali zinazotawala magumzo ya mchakato wa Katiba mpya hapa nchini, magumzo
yanayoendeshwa na makundi maalum kwa jazba na hata matusi. Hata hivyo nalazimika kutoa
maelezo ya ufafanuzi kuhusu upotoshaji mkubwa unaoendeshwa na baadhi ya watu kuhusu
Bunge Maalum. Nikiwa Mwenyekiti wenu ninao wajibu wa kuwafafanulia wananchi kuhusu
uhalali wa shughuli za Bunge Maalum linaloendelea na utaratibu wa shughuli zetu.
Ni
Rasimu ya Tume au la
Wapo wanaodai kuwa eti hapa Bungeni hatujadili Rasimu
ya Tume. Tuhuma hii haina ukweli hata kidogo. Msingi wa majadiliano yote tangu tumeanza
ni Rasimu ya Katiba iliyowasilishwa na Tume ya Katiba. Utaratibu ni kwamba pale ambapo
wajumbe wanaona panafaa kurekebishwa wanafanya hivyo. Maana ya rasimu ni andiko ambalo
halijajitosheleza bila kupata ithibati ya taasisi ya juu zaidi.
Anayekabidhiwa
rasimu anayo haki na mamlaka ya kuirekebisha. Vinginevyo kujadili rasimu hakuna sababu.
Itakuwa ni jambo la ajabu na lisilo na mantiki yoyote kuwa taasisi iliyopewa mamlaka
ya kujadili Rasimu ikishaijadili iiache ibaki kama ilivyokuwa wakati ilipowasilishwa!
Je
suala ni muundo wa Muungano tu? Maudhui ya Rasimu yanajumuisha baadhi ya masuala
muhimu yafuatayo: - Kuimarisha Muungano wetu kwa kuleta uwiano bora zaidi wa mamlaka
ya Zanzibar na Tanzania Bara ndani ya Muungano - Kuimarisha haki za binadamu ili
kuwawezesha raia wa kawaida kufaidi uhuru wa demokrasia bila ubabe na dhuluma -
Kuzuia wachache kufuja rasilimali za taifa bila kujali maslahi ya wengi na ya vizazi
vijavyo.
- Kujenga uwiano sahihi na wenye haki baina ya wanawake na wanaume
katika nafasi za uongozi. - Kubainisha hatua zenye kuleta matumaini mapya ya maendeleo
kwa makundi maalum ya vijana wakulima wadogo, wafugaji, wafanyakazi wa ngazi za kawaida,
walemavu, wafanya biashara wadogo na wajasiriamali wengine.
- Kuweka msingi
imara wa kutungwa kwa sheria kakamavu za kuzuia ukandamizaji wa raia, unyonyaji, wizi
wa mali ya umma, rushwa, hujuma dhidi ya uchumi na kuzuia mapato haramu na fedha chafu.
-
Kutambua haki za ardhi kwa wakulima, wafugaji na wajasiriamali wengine ili kupunguza
migongano na migogoro. - Kuweka Misingi ya utawala bora inayozingatia uadilifu,
sifa stahiki na ufanisi. - Kuwezesha kutungwa kwa sheria bora zaidi zitakazosimamia
chaguzi zilizo za haki na huru zaidi pamoja na kuwepo Tume za Uchaguzi zilizoboreshwa.
Zaidi
ya hivyo, yapo mapungufu katika Rasimu iliyopo kwa kuachwa masuala ya kuwezesha Serikali
za mitaa; kutoa maelekezo kuhusu masuala ya matumizi ya ardhi na rasilimali nyingine
za Taifa. Nini kinatuzuia kuiboresha Rasimu kwa kuyaongeza mambo haya ndani ya Katiba
kwa faida ya Taifa?
Yote haya ni masuala muhimu ambayo yamo ndani ya rasimu
na wakati wake wa kuyaweka sawa ndiyo huu. Pamoja na umuhimu wake suala la muundo
wa Muungano si suala la kutulazimisha tuyaahirishe mazuri yote yaliyomo katika Rasimu
tuliyopewa.
Uhalali wa Shughuli za Bunge Maalum
Pamoja na uhalali wa
kisheria wa Bunge hili Maalum kuendelea kufanya kazi zake, linao pia uhalali wa kisiasa
kutokana na sifa za uwakilishi wetu na pia maudhui yaliyomo ndani ya Rasimu. Kutofautiana
maoni hakuwapi hadhi tofauti baadhi ya wajumbe kujiona wao wana uhalali zaidi mbele
ya wananchi kuliko wenzao. Ndiyo maana utaratibu umewekwa wa kupiga kura na wa maridhiano.
Utamaduni mpya unaoanza kujengwa na baadhi ya viongozi wa jamii wa kususia mijadala
halali na kwenda nje kuelezea hoja za upande mmoja hauna nafasi katika Tanzania jamii
isiyotaka fujo na utengano. Wajumbe wa Bunge Maalum wanaoendelea na kazi mjini
Dodoma ni wateule wa Rais kwa niaba ya wananchi kwa kazi ya kutunga Katiba. Kazi hii
haiwezi kusitishwa kwa sababu tu wajumbe wachache wameisusia. Tutazingatia matakwa
ya sheria katika kufikia hatma ya mchakato wa Katiba.
Mabadiliko ya Kanuni Kamanilivyoeleza
hapo mwanzo, Rasimu ina jumla ya sura kumi na saba (17) zenye mambo mengi yenye maslahi
kwa Watanzania wote. Kwa muda tuliopewa wa siku sitini (60) isingewezekana kuikamilisha
kazi tuliyopewa ndani ya muda. Ikumbukwe kwamba kwa Kanuni zilivyo, kila sura mbili
zinahitaji siku tisa kuzifanyia kazi. Kwa njia hiyo, ingetuchukua siku takriban mia
moja thelathini (130) ili kuikamilisha kazi hii!
Pendekezo la msingi hapa
ni kwamba Kamati zetu kumi na mbili (12) zizingatie na kuzijadili sura kumi na tano
(15) za Rasimu na pia zikamilishe uandishi wa sura mbili zilizojadiliwa awali na ikibidi
ziongeze sura ambazo zitadhihirika kuwa ni muhimu.
Naamini mtiririko huu utatuwezesha
kuwa na mpangilio bora zaidi wa sura na ibara katika Katiba mpya. Tusingependa na
wala isingefaa kuomba tena muda wa ziada wa kazi ya Katiba ndio maana tunafanya mabadiliko
ya Kanuni. Kamati ya Uongozi iliyoketi Dar es Salaam tarehe 28 Julai 2014 imependekeza
yafanywe mabadiliko ya Kanuni za Bunge Maalum kuwezesha kazi ikamilike ndani ya muda
tuliopewa. Kwa hiyo nitawaomba tuyatafakari mapendekezo ya mabadiliko ya Kanuni na
hatimaye kuyapitisha ili ratiba ya kazi zetu iende sawa. Nitawaomba muikubali ratiba
iliyogawanywa leo na pia mkubali kuzibadilisha Kanuni kwa lengo nililolieleza hapa.
HITIMISHO:
Pamoja
na maoni ya kila namna yanayoendelezwa kujadili mchakato wa Katiba nje ya Bunge hili,
ni muhimu wahusika wapunguze jazba, chuki na upotoshaji. Bunge Maalum lisaidiwe kwa
mawazo chanya ili limalize kazi yake.
Sisi tuliomo humu katika Bunge Maalum
tuna wajibu wa kuifanya kazi yetu kwa umakini na kwa uadilifu ili kazi yetu iwe bora.
Tujadiliane kwa uungwana. Tofauti za mawazo zisitufanye tuingize chuki na maneno yasiyofaa.
Katika mabadiliko ya Kanuni nashukuru sasa Kiti kimepewa mamlaka ya kushughulikia
utovu wa nidhamu ndani ya wakati. Lakini ninaamini haitakuwa lazima kwangu mimi au
Makamu Mwenyekiti kutumia nguvu za mamlaka yetu ila tu pale itakapobidi.
Nawatakia
nyote Mkutano wenye mafanikio kwa maslahi mapana ya nchi yetu. MUNGU IBARIKI TANZANIA! Samuel
Sitta - MB MWENYEKITI BUNGE MAALUM LA KATIBA