Waandishi wa habari saidieni mchakato wa Uinjilishaji Mpya!
Shirikisho la Waandishi wa Habari Wakatoliki, UCAP, hivi karibuni limefanya mkutano
mkuu na wajumbe kumchagua Bwana George Sunguh kutoka Kenya kuwa ni Rais wa UCAP. Bwana
Desire Baiere kutoka DRC amechaguliwa kuwa Makamu wa kwanza wa Rais na Victoria Lugey
kutoka Ghana kuwa Makamu wa pili wa Rais. Wajumbe wamemchagua Bwana Rodrigue Dembele
kutoka nchini Mali kuwa katibu mkuu wa UCAP na Bwana Eleophas Tyenou kutoka Mali anakuwa
mtunza hazina.
Uchaguzi huu umefanyika katika maadhimisho ya mkutano mkuu wa
UCAP uliokuwa unafanyika Jimbo kuu la Bamako, nchini Mali. Askofu mkuu Jean Zerbo
wa Jimbo kuu la Bamako katika Ibada ya Misa takatifu, amewataka waandishi wa habari
kuhakikisha kwamba, wanasaidia utekelezaji wa mchakato wa Uinjilishaji Mpya, kwa kuwapatia
watu kweli za Kiinjili, ili kujenga na kuimarisha misingi ya haki, amani, upendo na
mshikamano wa kweli.
Anasema mkutano huu umefanyika nchini Mali ambako wakati
huu Mali inakabiliana na changamoto mbali mbali zinazotokana na kinzani za kijamii.
Mkutano huu umehudhuriwa pia na padre Janvier Yameogo, afisa kutoka Baraza la Kipapa
la Mawasiliano ya Jamii pamoja na Bwana Benedict Assorow, Msremaji mkuu wa Shirikisho
la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika na Madagascar, SECAM.