2014-08-04 10:36:25

Msiipatie Sudan ya Kusini kisogo, watu watakufa kwa njaa!


Askofu mkuu mstaafu Desmond Tutu wa Kanisa Anglikani, hivi karibuni, ameitaka Jumuiya ya Kimataifa kutoipatia kisogo Sudan ya Kusini na badala yake, ijitahidi kuhakikisha kwamba, Sudan ya Kusini inaungwa mkono katika masuala ya kisiasa, kimaadili na kiuchumi, ili amani, upatanisho na umoja wa kitaifa viweze kutawala. Sudan ya Kusini kwa sasa inakabiliwa na majanga makubwa yanayohitaji msaada na mshikamano na Jumuiya ya Kimataifa. Wananchi wengi wanakabiliwa na baa la njaa.

Takwimu zinaonesha kwamba, kuna watoto zaidi ya millioni moja wanakabiliwa na utapiamlo wa kutisha kutokana na machafuko ya kisiasa yanayoendelea nchini humo, licha ya jitihada za Jumuiya ya Kimataifa kuwataka wahusika kusitisha mapigano ambayo kwa sasa hayana mashiko wa tija, bali ni kielelezo cha uchu wa mali na madaraka.

Ikiwa kama Jumuiya ya Kimataifa haitafanikiwa kupeleka msaada wa chakula, watu wengi Sudan ya Kusini wanaweza kukumbwa na baa la njaa na madhara yake yatakuwa ni makubwa zaidi. Kumbe kuna haja kwa Jumuiya ya Kimataifa kusaidia mchakato wa kuokoa maisha ya wananchi wengi wa Sudan ya Kusini ambao kwa sasa wanakabiliwa na majanga ya maisha!







All the contents on this site are copyrighted ©.