Makanisa kujadili athari za mabadiliko ya tabianchi!
Baraza la Makanisa Ulimwenguni kuanzia tarehe 21 hadi tarehe 22 Septemba 2014, litafanya
mkutano kuhusu mabadiliko ya tabianchi utakaowahusisha viongozi wa kidini wapatao
30, huko New York, Marekani. Mkutano huu wa viongozi wa kidini unapania kutoa msukumo
na changamoto kwa viongozi wa kisiasa kulivalia njuga pasi na utani tatizo la mabadiliko
ya tabianchi linaloendelea kusababisha majanga kwa maisha ya watu na mali zao.
Mkutano huu
utafanyika siku chache kabla ya viongozi wa Jumuiya ya Kimataifa kuanza kushiriki
katika mkutano ulioitishwa na Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Bwana Ban Ki-Moon, ili
kupembua kwa kina na mapana mikakati inayopaswa kuchukuliwa na Jumuiya ya Kimataifa
katika kupambana na athari zinazosababishwa na mabadiliko ya tabianchi pamoja na kuweka
sheri itakayowabana ifikapo mwaka 2015.
Ni matumaini ya Baraza la Makanisa
Ulimwenguni kwamba, mchango wao utawaza kusikiwa na kufanyiwa kazi na Jumuiya ya Kimataifa
katika mkutano wa mabadiliko ya tabianchi uliopangwa kufanyika Mwezi Desemba, 2014
huko mjini Lima, nchini PerĂ¹ na baadaye mjini Paris, Ufaransa kunako mwa 2015. Baraza
la Makanisa Ulimwenguni katika mikutano hii linapenda kudai haki msingi za binadamu.
Baraza la Makanisa Ulimwenguni kwa zaidi ya miongo miwili limeendelea kusimama
kidete kulinda na kutetea haki msingi za binadamu, lakini wakati huu madhara ya mabadiliko
ya tabianchi yamefikia kiwango cha hali ya juu kabisa. Umefika wakati kwa viongozi
wa kisiasa kuweka uwiano wa kile wanachozungumza na utekelezaji wa maamuzi haya, jambo
linalohitaji ujasiri na maamuzi ya busara. Viongozi wa Jumuiya ya Kimataifa katika
maadhimisho ya mkutano wa mabadiliko ya tabianchi huko New York, Marekani, wanapaswa
kukumbushwa wajibu wao msingi wa kimaadili, unaopaswa kufanyiwa kazi.
Baraza
la Makanisa Ulimwenguni, linayataka Makanisa wanachama kuhakikisha kwamba, yanajifunga
kibwebwe kulinda na kutunza mazingira, kwa kuwa na mikakati ya pamoja, itakayoiwezesha
dunia, kuwa ni mahali bora zaidi pa kuishi kwa kuwarithisha vijana wa kizazi kipya
mazingira bora zaidi, kuliko mwelekeo wa sasa unaoendelea kukatisha watu tamaa ya
maisha kutokana na madhara makubwa ya mabadiliko ya tabia nchi.