2014-08-04 10:22:55

Kutolipa ada kutaharibu ubora wa elimu nchini Kenya


Askofu Maurice Muhatia Makumba, mwenyekiti wa Idara ya Elimu na dini na shuleni, Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya anasema kwamba, amri iliyotolewa na Serikali ya Kenya kuwataka wamiliki wa shule kutoa vyeti vya wanafunzi waliohitimu shule ni jambo ambalo linaweza kusababisha madhara makubwa katika ubora wa elimu inayotolewa nchini Kenya.

Askofu Makumba anaishauri Serikali kutafuta njia muafaka itakayowawezesha wazazi kulipia gharama ya elimu wanayodaiwa shuleni badala ya kutoa amri ambayo ina madhara makubwa katika ustawi na maendeleo ya sekta ya elimu nchini Kenya. Mwelekeo huu unaweza kuwachochea wazazi na walezi nchini Kenya kutolipa ada ya shule kwa watoto wao kwa makusudi kwani Serikali inawakingia kifua.

Shule zitakabiliwa na hali ngumu ya uendeshaji wa shughuli zake, ikiwa kama wazazi na walezi wanahamasishwa kutolipa ada ya shule matokeo yake uborwa wa elimu utapungua kwa kiasi kikubwa! Bodi za shule zipewe dhamana ya kuangalia wazazi wale ambao wanakabiliwa na hali ngumu ya maisha kiasi cha kushindwa kulipa ada, ili waweze kupewa msamaha. Serikali ya Kenya hivi karibuni imetangaza mkakati wa kutaka kupunguza gharama katika sekta ya elimu, ili kutoa fursa kwa wakenya wote kufaidi matunda ya elimu, wazo ambalo limebezwa na Umoja wa Walimu wa Shule za Msingi nchini Kenya, (KUPPET).







All the contents on this site are copyrighted ©.