Kumbu kumbu ya vita kuu ya kwanza ya dunia, ni changamoto ya kujikita katika msingi
wa haki na amani!
Baraza la Maaskofu Katoliki Canada linasema kwamba, Jumuiya ya Kimataifa inapoadhimisha
kumbu kumbu ya miaka mia moja tangu Vita kuu ya kwanza ya dunia ilipotokea, iwe ni
fursa kwa waamini na watu wenye mapenzi mema kuchuchumilia misingi ya haki, amani
na utulivu. Canada iliingia rasmi katika vita kuu ya kwanza ya dunia hapo tarehe 4
Agosti 1914 kwa kushirikiana na Uingereza dhidi ya Ujerumani iliyokuwa imevamia Ubelgiji.
Baraza
la Maaskofu Katoliki Canada linasema kuna haja ya watu kutofautisha kati ya vita na
madhara yake, kwani kimsingi haipaswi kabisa kusherehekea majanga yaliyosababishwa
na vita na badala yake kuwaheshimu Askari waliojitoa mhanga, ili kupambana na udhalimu,
wakakubali kupoteza maisha yao, kupata vilema na majeraha makubwa. Kwa maneno mengine,
Askari wamekuwa ni wahanga wa kwanza wa vita kuu ya kwanza ya dunia.
Waamini
wanaomboleza kutokana na vifo vyao na kuwaombea pumziko la amani, huko mbinguni, changamoto
kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema kujikita katika mchakato wa kutafuta,
kulinda na kudumisha misingi ya haki, amani na utulivu. Katika vita kuu ya kwanza
dunia wahudumu wa maisha ya kiroho walifanya kazi kubwa ya kuwasindikiza Askari pamoja
na familia zao; kiasi kwamba, wakawa kweli ni mwanga wa matumaini katika maeneo ambamo
mtutu wa bunduki ulikuwa unatawala.
Baraza la Maaskofu Katoliki Canada linasema,
amani ni jina jipya la maendeleo kama anavyokazia Mtumishi wa Mungu Papa Paulo VI.
Vita itaendelea kusababisha majanga makubwa katika maisha ya watu: Ukosefu wa fursa
za ajira, njaa, dhuluma na hali ya kukata tamaa. Kutokana na changamoto hizi, kuna
haja ya kujenga dunia ambamo haki na amani vinatawala.
Ni wajibu wa Wakristo
na watu wote wenye mapenzi mema kuwa ni mashahidi wa haki na amani; wafuasi na wamissionari
wa Mfalme wa amani, tayari kutangaza Injili ya Furaha kwa watu wa mataifa!