2014-08-02 08:49:29

Injili ya Kristo, Familia na Uhuru ni mambo yanayopaswa kushibana pasi na ukinzani!


Hati ya kutendea kazi kwa ajili ya Sinodi maalum ya Maaskofu kwa ajili ya Familia itakayoadhimishwa mjini Vatican kuanzia tarehe 5 hadi tarehe 19 Oktoba 2014 inaonesha utajiri mkubwa na uchambuzi wa kina uliofanywa kwa kuangalia matatizo, changamoto na fursa zilizopo katika maisha na utume wa Familia. RealAudioMP3

Mababa wa Sinodi watakuwa na fursa kwa kipindi cha miaka miwili kuweza kusali, kutafakari na hatimaye kutoa suluhu kwa changamoto ambazo zinaikumba familia katika ulimwengu wa utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia.

Matatizo na changamoto za kifamilia ni mwaliko kwa Mama Kanisa kuwatangazia tena watu Injili ya Familia, itakayogusa undani na vipaumbele vya maisha yao; uhuru na dhamana yao kwa kushiriki kikamilifu katika kazi ya uumbaji na malezi ya Kikristo kwa watoto wao sanjari na kudumisha misingi ya maadili na utu wema.

Watu watambue kwamba, wameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu jambo linalojenga mahusiano ya pekee na Mwenyezi Mungu anayeheshimu na kuthamini uhuru wa mwanadamu. Mwenyezi Mungu amempatia mwanadamu Amri na Maagizo yake ambayo yanapaswa kutekelezwa kwa dhati kama kielelezo cha upendo kwa Mungu. Uhuru ni dhana pevu ambayo ni sehemu ya utamaduni, Mapokeo na Mafundisho ya Kikristo.

Kila mtu anao uwezo wa kujichagulia mfumo wa maisha yake. Dhana ya uhuru wanasema wachunguzi wa mambo ya maisha ya kiroho na kimaadili “imechakachuliwa” na wajanja wachache kiasi kwamba inaanza kupoteza dira na mwelekeo wake. Uhuru unawapatia watu kuamua kuoa au kutokuoa; kuwa na watoto au kuendelea kula kuku kwa mrija pasi na bughuza na kero za watoto. Yote haya yanajikita katika dhana ya uhuru binafsi.

Utume wa familia unahitaji mwelekeo tofauti kabisa wa kutambua dhana ya uhuru, kwani hapa kunahitajika ukomavu wa kimaadili, utu na maisha ya kiroho mintarafu dhana ya uhuru wa mtu. Waamini watambue na kuthamini uhuru wao wa kuwa kweli ni Watoto wa Mungu, kwa kuepuka kishawishi cha ubinafsi kinachokwamisha hata wakati mwingine mahusiano ya kijamii. Uhuru wa waamini unapaswa pia kuzingatia Mafundisho ya Kanisa, Maadili na Utu wema.

Hapa kuna haja ya kuheshimu kanuni na sheria maadili, kwa kufuata dhamiri nyofu, ili kukuza na kudumisha mahusiano mema ndani ya jamii. Ndiyo maana Kanisa katika mapambazuko ya Millenia ya tatu ya Ukristo linataka kujikita zaidi katika Uinjilishaji Mpya unaozingatia ushuhuda wa maisha adili na matakatifu kwa kuwataka waamini kuwa kweli ni chachu ya kuyatakatifuza malimwengu.

Mchakato huu uwasaidie waamini kutambua umuhimu wa Mafundisho ya Kanisa na kujitahidi kuyamwilisha katika uhalisia wa maisha yao, kwa kutambua thamani kubwa ya uhuru ambao wamekirimiwa na Mwenyezi Mungu; uhuru unaowawajibisha katika maisha yao ya kiroho na kimaadili; uhuru pasi na mipaka ni utumwa na majanga katika maisha ya watu!








All the contents on this site are copyrighted ©.