Mtindo wa mawasiliano unaofanywa na Baba Mtakatifu Francisko na Maadhimisho ya Sinodi
mnaalum ya Maaskofu kwa ajili ya Familia ni kati ya mada kuu zilizochambuliwa hivi
karibuni na wadau na wasemaji wakuu wa Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Barani Ulaya,
katika mkutano wake uliofanyika mjini Lisbon, Ureno, kwa mwaliko wa Katibu mkuu wa
Baraza la Maaskofu Katoliki Ureno.
Padre Paul
Wuthe, msemaji mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Austria, akiwasilisha mada yake
kama sehemu ya utangulizi wa mkutano huu, amewawezesha wadau na wasemaji wakuu wa
Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Barani Ulaya, kufanya upembuzi yakinifu kuhusu mtindo
wa mawasiliano unaotumiwa na Baba Mtakatifu Francisko katika maisha na utume wake
kwa Kanisa la Kristo. Wajumbe wanakiri kwamba, Baba Mtakatifu amekuwa ni kati ya “vigogo”
katika vyombo vya mawasiliano ya jamii sehemu mbali mbali za dunia. Ni kiongozi ambaye
amekuwa na mvuto mkubwa kwenye mitandao ya kijamii.
Lakini ikumbukwe kwamba,
mtindo wake wa mawasiliano ni sehemu ya maisha yake ya kawaida yanayojengeka katika
maneno, lakini zaidi kwa njia ya ushuhuda wa maisha ambayo kwayo anajitahidi kuvunja
kuta za utengano kati yake na Watu wa Mungu. Ni kiongozi anayetaka kuwakumbatia wote,
ili kuwaonjesha huruma na upendo unaobubujika kutoka kwa Kristo na Kanisa lake. Baba
Mtakatifu anaonesha kwa njia ya matendo ukweli wa maisha yake kama Khalifa wa Mtakatifu
Petro, fursa na changamoto kwa Mama Kanisa kujikita katika majadiliano ya kina na
walimwengu.
Wajumbe wa mkutano huu wanakiri kwamba, Baba Mtakatifu Francisko
kwa mtindo wa maisha yake anaendelea kuwagusa wengi kutoka katika undani wa mioyo
yao, lakini pia ameleta mwamko mpya miongoni mwa waandishi na vyombo vya habari kitaifa
na kimataifa kuanza kuona mchango wa Kanisa katika ustawi, maendeleo na mafao ya wengi,
ikilinganishwa na miaka kadhaa iliyopita, ambako habari za Kanisa zilionekana kutokuwa
na mashiko wala mvuto katika vyombo vya habari! Kwa hakika wanasema, Papa Francisko
ni kiboko yao!
Wajumbe wanaonya kwamba, kuna haja ya kuwa waangalifu sana
kutokana na mtindo wa mawasiliano yanayojikita katika maisha na utume wa Baba Mtakatifu
Francisko. Ni kiongozi anayezungumza kidogo, kiasi kwamba, watu wasipokuwa makini
na kile anachozungumza, wanaweza kujikuita kwamba, wanapotoshwa na vyombo vya habari
ambavyo kwa sasa vinakimbilia na kufuatilia mambo katika ufupi wake na kwa haraka.
Huu ndio utamaduni unaofanyiwa kazi na vyombo vya mawasiliano ya kijamii!
Kumbe, kwa vyombo vya mawasiliano vinavyomilikiwa na kuendeshwa na Kanisa, havina
budi kuhakikisha kwamba, vinaendelea kutangaza maisha na utume wa Kanisa zima, kwa
kujikita katika kweli za Kiinjili na hata wakati mwingine, kwenda kinyume ni vyombo
vikuu vya upashanaji habari, ili kuondokana na mwelekeo mfinyu unaoweza kuugeuza mfumo
wa upashanaji habari wa Kanisa kujikita katika maisha ya mtu!
Mkutano wa wadau
na wasemaji wakuu wa Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Barani Ulaya, ulipata baraka ya
uwepo wa Padre Federico Lombardi, msemaji mkuu wa Vatican, gwiji katika masuala ya
habari, mtu ambaye kwa hakika ana uzoefu na mang’amuzi makubwa katika tasnia ya habari
ndani na nje ya Kanisa.
Kardinali Lorenzo Baldisseri, Katibu mkuu wa Sinodi
ya Maaskofu ameshiriki pia katika mkutano huu, ili kuwafunda wasemaji wakuu wa Mabaraza
ya Maaskofu Katoliki Barani Ulaya, kujiandaa kikamilifu katika maadhimisho ya Sinodi
maalum ya Maaskofu kuhusu familia, inayoadhimishwa hatua kwa hatua, kwa kuwashirikisha
Watu wa Mungu. Maadhimisho haya yalizinduliwa kwa kuwashirikisha waamini na watu wenye
mapenzi mema katika kujibu maswali dodoso kuhusu tunu msingi za maisha ya ndoa na
familia.
Hapa Kardinali Baldisseri anasema, si lengo la Kanisa kufanya utafiti
kuhusu maisha ya ndoa na familia kwa njia ya maswali dodoso, bali hii ni sehemu ya
mchakato wa utamaduni wa Kanisa kusikiliza kwa makini mchango unaotolewa na watoto
wake, ili hatimaye, kuibuka na mbinu mkakati wa shughuli za kichungaji zinazotekelezwa
na Mama Kanisa, kwa kukabiliana na changamoto hizi kwa imani na matumaini, ili kuendelea
kutangaza Injili ya Familia kwa watu wa mataifa, bila woga wala makunyanzi!
Sehemu
ya pili ya Maadhimisho ya Sinodi maalum ya Maaskofu kuhusu familia ni hati ya kutendea
kazi itakayotumiwa na Mababa wa Sinodi, hati ambayo inajulikana kama “Instrumentum
Laboris” ambayo imezinduliwa mjini Vatican hapo tarehe 26 Juni 2014. Hati hii itatumiwa
na Mababa wa Sinodi itakayoadhimishwa mjini Vatican kuanzia tarehe 5 hadi 19 Oktoba
2014. Awamu ya Pili ya Maadhimisho ya Sinodi hii yanatarajiwa kufanyika kunako mwaka
2015, Sinodi itakayoibua mbinu mkakati wa shughuli za kichungaji kwa familia ya binadamu.
Hapa Kanisa linapenda kukazia ukweli na uwazi, utume na uadilifu katika kusimamia
kweli za Kiinjili, kwa kusikiliza na kuamua kwa ujasiri, ili kuwatangazia watu wa
mataifa Injili ya Familia, chemchemi ya matumaini na maisha mapya. Mababa wa Sinodi
maalum ya Maaskofu kuhusu Familia watato mwelekeo wa Kanisa kuhusu maisha ya ndoa
na familia, changamoto ambayo imevaliwa njuga na Baba Mtakatifu Francisko tangu alipochaguliwa
kuliongoza Kanisa Katoliki.
Wasemaji wakuu wa Mabaraza ya Maaskofu Katoliki
Ulaya wamekumbushwa kwamba, hii si Sinodi ya Maaskofu wa Bara la Ulaya, bali ni Sinodi
inayolishirikisha Kanisa zima, kumbe ni kipindi cha kusali, kutafakari na kushirikishana
tunu mbali mbali za maisha ya ndoa na familia.
Kuna haja anasema Kardinali
Baldisseri kuwa na mwelekeo mpana zaidi badala ya kujikita katika masuala magumu na
nyeti katika maisha ya ndoa na familia na hatimaye kupuuzia ushuhuda unaotolewa na
Familia ya Mungu katika maisha ya ndoa na familia, kwani licha ya matatizo, changamoto
na fursa mbali mbali zilizopo, kuna familia ambazo kweli zimekuwa ni kielelezo cha
Injili ya Familia katika uhalisia wa maisha yao ya kila siku, hawa ni watu wakupongezwa
na kutiwa shime, ili waweze kusonga mbele kwa imani na matumaini.
Mkutano
wa wasemaji wakuu kutoka Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Barani Ulaya, ulihudhuriwa
pia na Bwana Benedict Assorow, msemaji mkuu wa Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu
Katoliki Afrika na Madagascar, SECAM.