2014-08-02 09:27:10

Familia bora ni kitalu cha miito mitakatifu!


Askofu mkuu Paul Bui Van Doc wa Jimbo kuu la Hochiminh Ville, nchini Vietnam anasema, mikakati makini ya shughuli za kichungaji kwa ajili ya familia, inayotoa kipaumbele cha kwanza kwa maisha ya Sala na Sakramenti za Kanisa, umuhimu wa Neno la Mungu na ushuhuda adili wa maisha ya Kikristo ni chemchemi kubwa ya miito mitakatifu ndani ya Kanisa Katoliki nchini Vietnam. RealAudioMP3

Miito mitakatifu, mapadre na watawa wema, watakatifu na wanyofu wa moyo wanazaliwa kutoka katika familia za Kikristo zinazowajibika barabara na wala si bahati mbaya kwamba, Kanisa linaendelea kukazia umuhimu wa shughuli, mikakati na utume wa familia hasa katika nyakati hizi ambamo familia inakumbana na changamoto nyingi katika maisha na utume wake.

Askofu mkuu Paul Bui Van Doc ambaye pia ni Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Vietnam anasema, Kanisa nchini humo linaendelea kujielekeza zaidi katika majiundo makini na endelevu kwa Mapadre na Majandokasisi. Vietnam ina Waseminari wakuu 250 na kwamba, miito inazidi kuchanua na kukua kama mitende ya Lebanon. Vietnam ina jumla ya seminari nane zinazowahudumia Waseminari 3, 000 katika Mashirika ya kitawa na kazi za kitume pamoja na Majimbo Katoliki nchini Vietnam.

Askofu mkuu Van Doc anasema, majiundo na malezi ya Kipadre Seminarini yanakabiliwa na changamoto kubwa kutokana na maendeleo ya sayansi na teknolojia pamoja na athari za utandawazi zinazowajengea watu moyo wa ubinafsi na kujitafuta wenyewe, hali inayochangia pia kukua na kushamiri kwa ukanimungu. Ukuaji wa miito mitakatifu nchini Vietnam ni matunda ya majiundo makini ya maisha na utume wa Familia za Kikristo kama Kanisa dogo la nyumbani na kitalu cha miito.

Pale ambapo kuna familia zinazojikita katika utakatifu na maisha adili, hapo kuna uwezekano mkubwa wa kupata Mapadre, Watawa na Raia wema na waadilifu; watu wenye moyo na ari ya kujisadaka kwa jili ya jirani zao. Baraza la Maaskofu Katoliki Vietnam linaendelea kuwekeza kwa kiwango kikubwa katika utume wa familia, ili familia za Kikristo ziweze kuwajibika katika maisha na utume wake ndani na nje ya Kanisa.








All the contents on this site are copyrighted ©.