Vunjilieni mbali kuta za utengano, ili kujenga na kuimarisha upendo na msamaha!
Kardinali Rodriguez Maradiaga, Rais wa Shirikisho la Mashirika ya Misaada ya Kanisa
Katoliki Kimataifa, Caritas Internationalis katika tafakari yake ya kina kuhusu vita
na machafuko yanayoendelea huko Mashariki ya Kati, anamwomba Yesu asaidie watu kuvunja
kuta za kinzani, ili kujenga na kuimarisha mshikamano wa upendo, kwa kujifunza kutoka
kwa jirani zao, huku wakipania kuwasamehe wale waliowakosea.
Ni maneno ya
Mtakatifu Yohane wa XXIII katika Waraka wake wa kichungaji Amani Duniani, Pacem in
Terris aliyoyatoa zaidi ya miaka hamsini iliyopita, lakini bado yana umuhimu wa pekee
wakati huu ambapo kuna vita na kinzani zinazoendelea sehemu mbali mbali za dunia.
Kuna zaidi ya watu millioni mbili ambao wamekumbwa na madhara ya vita huko Mashariki
ya Kati. Ni watu ambao hawana uhakika wa usalama wa maisha yao, watu wasiokuwa na
hatia wanaendelea kupoteza maisha yao huko Ukanda wa Gaza, kiasi kwamba, matumaini
ya kupata amani yanaendelea kufifia kila kuchwapo!
Jambo la kustikisha ni kuona
kwamba, uwanja wa vita ni sehemu ambayo imesheheni watu na hospitali zimefurika kwa
watu waliojeruhiwa na maiti za watu wasiokuwa na hatia. Watu wanalipuliwa wakiwa shuleni,
mahali ambapo wamekimbilia kutafuta usalama wa maisha yao.
Caritas Internationalis
imeziomba pande zinazohusika kusitisha vita, kama sehemu ya kwanza ya mchakato unaopania
ujenzi wa amani inayojikita katika majadiliano ya kina huko Mashariki ya Kati. Ni
mwanzo wa hija ngumu ya upatanisho inayokijita katika maisha ya mtu binafsi, changamoto
kwa Israel na Hamas kuweka silaha chini na kuanza mchakato wa majadiliano. Hii ni
vita ya tatu katika kipindi cha miaka mitano iliyopita.
Wapalestina wanaishi
katika mazingira magumu kwani kwa sehemu kubwa maisha yao yanategemea misaada kutoka
katika Jumuiya ya Kimataifa na kwamba, hakuna fursa za ajira. Kuna haja ya kuwapatia
wananchi wa Palestina fursa ya kuokoa maisha yao kwa kujikita katika mchakato wa ujenzi
wa amani inayokumbatiwa kwa ujasiri, majadiliano na kuheshimiana. Caritas inaombea
amani na utulivu huko Mashariki ya Kati na inaendelea kutoa msaada wa hali na mali
hata kwa kuhatarisha maisha ya wafanyakazi wake.
Jumuiya ya Kimataifa inafanya
kumbu kumbu ya miaka mia moja tangu ilipoanza vita kuu ya kwanza ya dunia, hata katika
shida na mahangaiko ya wananchi wa Palestina na Israeli, Kardinali Oscar Rodriguez
Maradiaga anasema, mioyo ya wananchi hawa inapaswa kuwa huru, ili kukumbatia misingi
ya haki na amani.