2014-08-01 10:57:34

Bado kuna idadi kubwa ya wahamiaji na wakimbizi wanaokufa maji baharini!


Kardinali Antonio Maria VegliĆ², Rais wa Baraza la Kipapa la shughuli za kichungaji kwa ajili ya wahamiaji na watu wasiokuwa na makazi maalum anasema kwamba, bado kuna idadi kubwa ya wahamiaji wanaokufa maji wakijaribu kutafuta maisha bora zaidi Barani Ulaya.

Wahamiaji wanapaswa kupewa uzito wa pekee kwa kuwapatia fursa ya kuishi kama binadamu, wakati huo Jumuiya ya Ulaya ikiendelea kutekeleza dhamana na wajibu wake. Watu wajitahidi kujenga jamii inayojikita katika upendo na mshikamano, kwa kuonesha ukarimu kwa watu wanaoteseka kutokana na majanga mbali mbali ya maisha!

Baba Mtakatifu Francisko anaichangamotisha Jumuiya ya Kimataifa kuhakikisha kwamba, utu na heshima ya binadamu vinapewa kipaumbele cha kwanza na kwamba, kuna haja kwa nchi mbali mbali kushirikiana na kusaidiana katika kuwahudumia wahamiaji na wakimbizi, ili kujenga dunia ambayo inasimikwa katika misingi ya haki, mshikamano na ubinadamu. Kuna watu wanaokimbia vita, dhuluma na nyanyaso mbali mbali; watu ambao wamegeuzwa kuwa ni mtaji wa wafanyabiashara wasiokuwa na utu wala dhamiri nyofu.

Watu wawajibike kwa ajili ya kuwasaidia wahamiaji na wageni, kwa kubadili tabia na mwelekeo wa maisha; ili kuguswa na mahangaiko ya wahamiaji na wageni; kwa kujenga na kuimarisha utamaduni wa watu kukutana na kusaidiana kwa kutambua haki na wajibu uliopo. Jamii ijipushe anasema Kardinali VegliĆ² kujikita katika utandawazi usioguswa na mahangaiko ya wengine. Sheria za kitaifa na kimataifa zitumike katika kuwahudumia wahamiaji na wakimbizi.

Kuna umati mkubwa wa wahamiaji na wakimbizi kutoka katika nchi zilizoko kwenye Pembe ya Afrika na Mashariki ya kati; watu wanaotafuta hifadhi ya maisha, kumbe wanapaswa kusaidiwa. Jumuiya ya Kimataifa iwe na mikakati ya muda mfupi na mrefu katika kuwahudumia wahamiaji na wakimbizi; kwa kutafuta mafao ya wengi na kudumisha uhuru.

Wahamiaji wanaweza kuwa ni fursa nzuri katika kukuza na kuendeleza uchumi, ingawa kwa sasa wanaoenekana kuwa kama tishio la usalama kwa nchi za Ulaya. Upendo na ukarimu ni mambo ambayo yanapaswa kuvaliwa njuga kwa wakati huu, ili kuwasaidia wakimbizi na wahamiaji.







All the contents on this site are copyrighted ©.