2014-08-01 09:45:00

Albania wakristo walikiona cha mtema kuni, lakini wakasimama imara katika imani na umoja!


Askofu mkuu Rrok Mirdita wa Jimbo kuu la Tirana, Albania anasema kwamba, hija ya kitume ya Baba Mtakatifu Francisko nchini humo, Jumapili tarehe 21 Septemba 2014, ni alama ya shukrani kwa Baba Mtakatifu kwa kutambua mchango mkubwa uliotolewa na Wakristo wa Albania kwa kusimama imara katika imani na kuendelea kushikamana na Khalifa wa Mtakatifu Petro, katika umoja, upendo na uaminifu; wakati ambapo Khalifa wa Mtakatifu Petro alipokuwa anahesabiwa kuwa ni kati ya maadui wakubwa wa Albania.

Baba Mtakatifu anatembelea Albania ili kuwaimarisha ndugu zake katika imani, matumaini na mapendo pamoja na kutoa heshima yake kwa wafiadini wa Albania, waliojisadaka kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake. Wananchi wa Albania kwa ujumla wao, lakini kwa namna ya pekee kabisa, waamini wanamsubiri kwa shauku kubwa Baba Mtakatifu Francisko, ili kukutana na kuzungumza naye. Watu wana imani na matumaini makubwa kwa Baba Mtakatifu Francisko.

Askofu mkuu Mirdita anasema katika mahojiano na Radio Vatican kwamba, wengi walidhani kwamba, kuanguka kwa Ukomunisti nchini Albania kungesababisha kinzani za kidini, lakini mambo yamekwenda kinyume kabisa cha wasi wasi na mashaka ya wengi, kwani hadi leo hii Albania ni kielelezo cha watu wa imani na dini mbali mbali wanaoishi kwa amani na utulivu, lakini ni amani ambayo imefikiwa kwa watu wengi kujisadaka na matunda yake, sasa yanafurahiwa na wengi. Wananchi wa Albania wamejifunza kwamba, mtu anaweza kuwa mwaminifu katika dini yake na kuwaheshimu waamini wa dini nyingine pia.

Itakumbukwa kwamba, imepita takribani miaka 21 tangu Mtakatifu Yohane Paulo II alipotembelea Albania, akawapatia faraja na changamoto ya ujenzi wa Kanisa la Kristo kwa kuwaweka wakfu Maaskofu wanne wa kwanza nchini Albania baada ya kuanguka kwa utawala wa Kikomunisti. Tangu wakati huo, Idadi ya Mapadre, Watawa na Waamini walei imeongezeka maradufu na kwamba, Mashirika ya Kimissionari yamepewa fursa kubwa katika Uinjilishaji wa kina, unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili.

Kuna maendeleo makubwa katika maisha na utume wa Kanisa, lakini changamoto pia bado zipo. Kwa mfano: Rushwa imekuwa ni janga na kitaifa, umaskini, ukosefu wa fursa za ajira na haki msingi za binadamu pamoja na ongezeko la makosa ya jinai.

Ikumbukwe kwamba, hii ni hija ya kwanza ya kitume kufanywa na Baba Mtakatifu Francisko Barani Ulaya na Albania ni nchi ya kwanza kubahatika kutembelewa na Papa Francisko. Nchini Albania, familia bado ina nguvu, wazee wanaheshimiwa na kuthaminiwa, waamini wa dini mbali mbali wanaishi kwa amani na utulivu na kwamba, kuna haki jamii inayotawala kati ya watu. Hija ya kitume ya Baba Mtakatifu nchini Albania inaongozwa na kauli mbiu "Pamoja na Mwenyezi Mungu, katika matumaini yasiyodanganya". Nembo ya hija hii inaonesha Wakristo wanaoibuka kutoka katika damu ya mashahidi na kuendelea kutembea na Msalaba kama kinga yao.







All the contents on this site are copyrighted ©.