2014-07-31 10:13:23

Ujumbe wa AMECEA kwa Familia ya Mungu na Watu wote wenye mapenzi mema


Mshikamano wa Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika Mashariki na Kati AMECEA kwa watu wanaokabiliwa na majanga mbali mbali, umuhimu wa familia kama kiini cha maisha ya kijamii, Uinjilishaji mpya na changamoto zake, umuhimu wa matumizi sahihi ya teknolojia ya mawasiliano ya kisasa katika mchakato wa Uinjilishaji mpya, watoto na vijana, wataalam wa Kikatoliki, seminari na nyumba za malezi, vitendo vya kigaidi na uvunjifu wa misingi ya haki na amani, ni kati ya mambo makuu yaliyojitokeza katika ujumbe wa AMECEA kwa Familia ya Mungu na kwa ajili ya watu wenye mapenzi mema katika nchi za Afrika Mashariki na Kati.

Mkutano mkuu wa 18 wa AMECEA uliokuwa unafanyika mjini Lilongwe, Malawi umeongozwa na kauli mbiu "Uinjilishaji kwa njia ya wongofu na ushuhuda wa imani ya Kikristo". AMECEA kwa namna ya pekee inamshukuru Baba Mtakatifu Francisko kwa changamoto zake katika mchakato wa Uinjilishaji mpya, mshikamano na upendo kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii. AMECEA inaishukuru Serikali ya Malawi kwa ukarimu na ushiriki wake mkamilifu katika maadhimisho ya mkutano mkuu wa AMECEA. Wanawashukuru wadau mbali mbali waliojisadaka kwa ajili ya AMECEA.

AMECEA inapenda kuonesha mshikamano wake wa dhati na wananchi wote ambao wanakabiliwa na hali ngumu ya maisha kutokana na vita, kinzani na migogoro ya kijamii. Ni matumaini ya AMECEA kwamba, suluhu ya amani ya kudumu itapatikana katika maeneo ambayo bado kuna vita na kinzani. Wananchi wanachangamotishwa kujikita katika misingi ya haki, amani, upatanisho na umoja wa kitaifa.

AMECEA katika ujumbe wake inabainisha kwamba, Familia ni kiini cha maisha ya kijamii, lakini kwa sasa inakabiliwa na matatizo na changamoto nyingi, ikiwa ni pamoja na: kuvunjika kwa misingi ya maadili na utu wema, mashambulizi dhidi ya familia, umaskini na ukosefu wa fursa za ajira. AMECEA kwa upande wake inasema, itaendelea kuzivalia njuga changamoto zote hizi ili kuimarisha Familia kama Kanisa dogo la nyumbani. Kanisa litaendelea kuzisaidia familia zilizovunjika na zile ambazo kwa sasa zinakabiliwa na hali ngumu ya maisha na kwamba, inalaani unyanyasaji unaofanywa majumbani.

AMECEA inapenda kukazia kuhusu umuhimu na udumifu wa ndoa kati ya mwanaume na mwanamke kwa ajili ya kushiriki katika kuzaa na kulea watoto. AMECEA inalaani harakati zozote zile zinazotaka kupindisha ukweli kuhusu taasisi ya familia. Maisha ya kifamilia hayana budi kuheshimiwa, kulindwa na kudumishwa, ili kujenga misingi ya haki, amani na utulivu.

Maaskofu wa AMECEA wanalaani ndoa za watu wa jinsia moja, jambo linalokwenda kinyume cha ubinadamu na kanuni maadili. Familia inapaswa kulindwa kwa gharama zote, ili kuiwezesha kuwa kweli ni chombo cha Uinjilishaji mpya, ambao ni wa Kiafrika na Kikristo kweli! AMECEA inaendelea kuvuta subira ili kupokea matunda ya maadhimisho ya Sinodi maalum ya Maaskofu kwa ajili ya familia.

AMECEA inasema, katika maadhimisho ya mkutano wake mkuu, imepembua kwa kina na mapana changamoto na fursa za uinjilishaji mpya kwa kuangalia jinsi ambavyo Wamissionari walivyotekeleza utume huu na kwamba, mihimili ya Uinjilishaji inahamasishwa kuendelea kuwa ni waaminifu kwa Kristo na Kanisa lake. Katekesi makini, toba na wongofu wa ndani, tasaufi ya kweli na ushuhuda thabiti ni mambo msingi kwa Wakristo ndani na nje ya AMECEA. Wakristo wanahamasishwa kushiriki kikamilifu katika Jumuiya ndogo ndogo za Kikristo, kama sehemu muafaka za kushirikishana mang'amuzi ya imani.

Mababa wa AMECEA wamekazia umuhimu wa matumizi sahihi ya teknolojia ya mawasiliano katika mchakato wa kutangaza Habari Njema ya Wokovu. Watoto na vijana walindwe na kufundwa kikamilifu ili waweze kuwa ni vyombo vya haki na amani. Wanaziomba Serikali katika nchi za AMECEa kuwekeza zaidi katika elimu na fursa za ajira ili kuwajengea vijana uwezo wa kuishi kwa heshima. Kanisa kwa upande wake, litaendelea kuwekeza katika majiundo makini ya watoto na vijana.

Vyuo vikuu na taasisi za elimu ya juu zinazomilikiwa na kuendeshwa na Kanisa ni mahali pa kuwakutanisha watu mbali mbali na kwamba, kwa njia ya elimu, Kanisa linaendelea kuwainjilisha watu na kuwajengea uwezo wa kuwajibika barabara katika jamii zao. Wanafunzi katika taasisi hizi wapewe kanuni maadili na maisha ya kiroho na kwamba, viongozi wa maisha ya kiroho watekeleze dhamana hii hata nje ya maadhimisho ya Ibada ya Misa Takatifu.

Wanataaluma Wakatoliki wataendelea kufundwa katika imani, ili waweze kuwa kweli ni mashahidi amini na muhimu wanapotekeleza dhamana yao Barani Afrika. Wanaalikwa kushiriki kikamilifu katika mchakato wa Uinjilishaji mpya. Seminari na nyumba za malezi ni sehemu muhimu sana za kufunda mihimili ya Uinjilishaji na kwamba, hapa ni mahali pa kupewa kipaumbele cha kwanza, ili kukidhi mahitaji kwa kuendelea kusoma alama za nyakati. Walezi makini wanatakiwa Seminarini na kwenye nyumba za malezi.

AMECEA inasikitika kusema kwamba, kwa miaka mingi nchi za AMECEA zimekuwa zilifurahia amani na utulivu, lakini vitendo vya kigaidi na uvunjifu wa amani vinaendelea kutishia usalama na maisha na wananchi wengi wa AMECEA. Wanaziomba Serikali kuhakikisha kwamba, zinashirikiana na Jumuiya ya Kimataifa ili kukomesha vitendo vya kigaidi. Wanawahimiza waamini na watu wote wenye mapenzi mema kujikita katika mchakato utakaosaidia kujenga na kudumisha uhuru wa kidini, uhuru wa dhamiri pamoja na kuheshimu haki msingi za binadamu, kama msingi mkuu wa amani na utulivu.

AMECEA inapongeza Serikali zile ambazo zimekuwa mstari wa mbele kulinda na kudumisha uhuru wa kuabudu. Inalaani mashambulizi yanayofanywa na waamini wenye misimamo mikali ya kidini na kiimani, changamoto kwa watu kuheshimiana na kuendeleza majadiliano ya kidini na kiekumene. AMECEA inapenda kuungana na wote waliokumbwa na majanga mbali mbali wakati walipokuwa wanaadhimisha mkutano mkuu wa kumi na nane huko Lilongwe, Malawi. Wanawatakia kheri na baraka tele!

Ujumbe wa AMECEA kwa Familia ya Mungu na watu wenye mapenzi mema, umetiwa sahihi kwa mara ya kwanza na Askofu mkuu Berhaneyesus Souraphiel, Mwenyekiti mpya wa AMECEA.







All the contents on this site are copyrighted ©.