2014-07-31 10:44:13

Maaskofu wanaozungumza Kireno kukutana tena 2016 huko Aparecida, Brazil


Mkutano wa Maaskofu Katoliki wanaozungumza Kireno uliokuwa unafanyika mjini Luanda, Angola umehitimishwa hivi karibuni na kwamba, imekuwa ni fursa makini katika kukuza, kujenga na kuimarisha umoja na mshikamano katika utekelezaji wa mikakati mbali mbali ya shughuli za kichungaji kwa Makanisa yanayozungumza Kireno. Maaskofu hawa wameamua kwamba, mkutano wa kumi na mbili, utafanyika kuanzia tarehe 23 hadi tarehe 28 Julai 2016, huko Aparecida, Brazil.

Katika mkutano huu, Maaskofu wanaozungumza lugha ya Kireno kutoka katika nchi nane duniani, wameweza kushirikishana kuhusu mang'amuzi, changamoto na vipambaule katika maisha na utume wa Kanisa kutoka katika nchi zao, mintarafu mwanga wa Waraka wa kitume ulioandikwa na Baba Mtakatifu Francisko, Injili ya Furaha.

Waraka huu anasema Askofu mkuu Gabriel Mbilingi, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Angola, Sao Tome na Principe kwamba, umekuwa ni kiini cha majadiliano ya Maaskofu wanaozungumza Kireno, tukio ambalo limewashirikisha hata waamini walei, kwani lilifanyika kwenye Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha Angola.

Maaskofu wanatambua umuhimu na dhamana ya waamini walei katika maisha na utume wa Kanisa. Wanawataka waamini walei kujitosa kimasomaso kwa ajili ya kushuhudia tunu msingi za maisha ya Kikristo kama njia ya kuyatakatifuza malimwengu. Maaskofu pia wamegusia umuhimu wa taasisi za elimu ya juu na vyuo vikuu vinavyomilikiwa na kuendeshwa na Kanisa Katoliki katika mchakato wa Uinjilishaji mpya; hali ya miito ya kipadre na kitawa pamoja na changamoto zake; wameangalia pia majadiliano ya kidini na kiekumene kama njia muafaka ya Uinjilishaji mpya.







All the contents on this site are copyrighted ©.