Kanisa linataka kuwasilikiza wanafamilia kwa moyo wote!
Kardinali Lorenzo Baldisseri, Katibu mkuu wa Sinodi za Maaskofu anabainisha kwamba,
Mama Kanisa anapoendelea kukabiliana na changamoto mbali mbali katika maisha ya ndoa
na familia anapenda kwa namna ya pekee kujikita katika hija ya kusikiliza Neno la
Mungu pamoja mahangaiko ya watu kutoka sehemu mbali mbali za dunia.
Kwa mara ya
kwanza katika historia ya Kanisa Katoliki, watu wamepewa fursa ya kutoa maoni yao
ili kujenga utamaduni wa mantiki ya Kanisa kusikiliza kwa makini na hatimaye kutenda
kwa ujasiri. Kanisa kama Jumuiya ya waamini kwa kushirikiana na watu wote wenye mapenzi
mema ili kutafuta majibu muafaka ya changamoto zinazoendelea kumkabili mwanadamu katika
maisha ya ndoa na familia limeamua kufanya maadhimisho ya Sinodi, kipindi cha kusali,
kutafakari na kutenda. Watu wana matatizo, wanazo changamoto za maisha, wana machungu
na wasi wasi, lakini pia wana matumaini na furaha wanayosali na kuwashirikisha wengine.
Kardinali Baldiselli anasema, mantiki hii imeliwezesha Kanisa kupambanua tema
itakayofanyiwa kazi na Mababa wa Sinodi maalum ya Maaskofu kwa ajili ya familia itakayoadhimishwa
mjini Vatican kuanzia tarehe 5 hadi tarehe 19 Oktoba 2014. “Changamoto za kifamilia
mintarafu Uinjilishaji mpya” ndiyo kauli mbiu inayoongoza maadhimisho haya, ambayo
yamepata baraka ya pekee kutoka kwa Baba Mtakatifu Francisko anayelihamasisha Kanisa
kusikiliza kwa moyo, huruma na upendo wa kibaba.
Sinodi ya maalum ya Maaskofu
kwa ajili ya familia, itakuwa ni hija ya Familia ya Mungu kutembea kwa pamoja. Tayari
kazi ya kukusanya na kuhariri majibu yaliyokusanywa na kuhaririwa na Mabaraza ya Maaskofu
mahalia imekamilika na hapo tayari kuna Hati ya kutendea Kazi ijulikanayo kwa lugha
ya Kilatini, Instrumentum Laboris.
Baba Mtakatifu Francisko ameamua kwamba,
maadhimisho ya Sinodi yatakuwa katika awamu kuu mbili: Awamu ya kwanza itakuwa ni
kusikiliza na kupokea ushuhuda kutoka kwa watu mbali mbali, ili kuishi na kutangaza
kwa ari na moyo mkuu Injili ya Familia. Awamu ya Pili ya Maadhimisho ya Sinodi hii
yatafanyika kunako mwaka 2015 ili kubainisha mwongozo wa jumla utakaotumika katika
utekelezaji wa mikakati ya shughuli za kichungaji kwa ajili ya binadamu na familia
kwa ujumla.
Awamu zote mbili ni mwendelezo wa maadhimisho ya tukio hili kubwa
katika maisha na utume wa Kanisa kama sehemu ya utekelezaji wa dhamana ya Uinjilishaji
mpya, changamoto inayovaliwa njuga kwa sasa na Mama Kanisa mintarafu mafundisho ya
Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican. Kanisa ambalo ni mwanga wa mataifa, linatumwa kutangaza
furaha na matumaini kwa kuwasaidia waamini na watu wote wenye mapenzi mema kumwilisha
Injili ya Furaha katika maisha yao.
Katika maadhimisho haya kutakuwa na hati
tatu zitakazotolewa. Hii inatokana na ukweli kwamba, Jamii ya mwanadamu kwa sasa inahitaji
kuangaliwa kwa jicho makini zaidi, ili kubainisha changamoto za kichungaji na hatimaye,
kuzifanyia kazi. Kati ya changamoto hizi ni ndoa mchanganyiko zinazofungwa kati ya
Wakatoliki na waamini wa dini nyingine; familia ya mzazi mmoja, ndoa za wake wengi,
mila na tamaduni zilizopitwa na wakati; myumbo wa familia kiasi cha kusambaratika
hata katika uchanga wake; kuyumba kwa mahusiano ya ndoa na matokeo yake ni watu kukimbilia
katika “nyumba ndogo” au kwenda “mchepuko” kama wanavyosema waswahili.
Katika
maisha ya ndoa na familia bado mfumo dume unatawala sehemu nyingi za dunia na kuna
baadhi ya nchi wanawake wanashika usukani. Wahamiaji na changamoto za maisha ya ndoa
na familia; dhana ya familia na madai ya ndoa za jinsia moja na dhamana ya malezi
kwa watoto wanaoasiwa ni kati ya matatizo yanayoikabili familia ya mwanadamu.
Vyombo
vya mawasiliano ya jamii: uzuri na madhara yake katika tunu msingi za maisha ya ndoa
na familia. Tatizo la uzazi wa chupa, tafsiri mpya kuhusu haki msingi za binadamu
na sheria zake; ukanimungu na Sakramenti ya ndoa na Upatanisho kutopewa umuhimu unaostahili.
Yote haya ni mambo ambayo yamejadiliwa kwa kina na mapana katika Hati ya Kutendea
Kazi, Instrumentum Laboris.
Kardinali Lorenzo Baldisseri, Katibu mkuu wa Sinodi
za Maaskofu anasema, hii ni kazi ya nguvu iiyofanyika kuanzia mwaka 2013 inagusa kwa
namna ya pekee mada kuhusu maisha ya ndoa na familia. Kwa mara ya kwanza waamini na
watu wenye mapenzi mema wameshiriki kwa wingi kuchangia katika maswali dodoso yaliyotolewa.
Maadhimisho ya Sinodi yatawashirikisha Watu wa Mungu, ili kuonesha umoja na mshikamano
katika tofauti inayojikita katika karama, mapaji, utume na ufahamu wa mambo.
Imehaririwa
na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.