Sitisheni biashara ya silaha kwa Syria, ili kukomesha vita!
Shirika la kutetea amani kimataifa, Pax Christi, linauomba Umoja wa Mataifa kupiga
rufuku biashara ya silaha nchini Syria na kuanzisha tena mchakato wa majadiliano yanalenga
kutafuta amani kwa kuzihusisha pande zote zinazohusika katika mgogoro huu.
Huu
ndio mkakati pekee utakaoiwezesha Syria kusitisha vita na amani kuanza kutawale tena,
chini ya udhibiti wa Umoja wa Mataifa. Katika vita hii, kuna mataifa ambayo yanaendelea
kufanya biashara ya silaha na Syria, kiasi kwamba, maafa yanazidi kuongezeka siku
hadi siku.
Pax Christi linasema, licha ya Jumuiya ya Ulaya kupiga rufuku biashara
ya silaha na Syria, lakini Syria imeendelea kununua silaha na kwamba, jitihada za
Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuanzia mwaka 2011 halijafanikiwa kupata suluhu
ya kisiasa kuhusiana na vita huko Syria. Takwimu zinaonesha kwamba, zaidi ya watu
laki moja na sitini wamekwishafariki dunia na wengine laki sita hawana makazi maalum
na kwamba, nusu ya wananchi wa Syria wamegeuka kuwa wakimbizi hata katika nchi yao
wenyewe.
Pax Christi inaitaka Jumuiya ya Kimataifa kusitisha kabisa biashara
ya silaha nchini Syria na kuanzisha mara moja mchakato wa amani na upatanisho wa kitaifa.
Pax Christi inaupongeza Umoja wa Mataifa kwa kumteuwa Bwana Staffan de Mistura kuwa
mwakilishi maalum wa Umoja wa Mataifa nchini Syria. Ulinzi na usalama kwa wananchi
wa Syria ni jambo linalopaswa kupewa kipaumbele cha kwanza. Watu wanaokimbia vita
na dhuluma waoneshwe ukarimu na Jumuiya ya Kimataifa.