2014-07-30 09:32:01

Jumuiya ya Kimataifa inahamasishwa kusaidia mchakato wa kusitisha vita huko Mashariki ya Kati!


Askofu mkuu Dominique Mamberti, Katibu mkuu wa mambo ya nchi za nje na ushirikiano wa kimataifa mjini Vatican anasema kwamba, Sekretarieti ya Vatican imewatumia ujumbe wa maandishi Mabalozi na wawakilishi wa nchi na mashirika mbali mbali ya kimataifa mjini Vatican ili kuonesha wasi wasi na hofu ya Baba Mtakatifu Francisko kuhusu kuteteleka kwa amani huko Mashariki ya Kati.

Wakristo wanaendelea kuteseka na kudhulimiwa; Makanisa na nyumba za Ibada zinaendelea kuharibiwa na kwamba, wakristo hawana nafasi tena ya kuadhimisha Ibada ya Misa takatifu hata katika nchi yao wenyewe! Ikumbukwe kwamba, Wakristo huko Iraq kama ilivyo kwa nchi nyingine huko Mashariki ya Kati, wamekuwepo huko zaidi ya miaka elfu na kwamba, wamechangia kwa kiasi kikubwa katika ustawi na maendeleo ya Mashariki ya Kati. Wakristo wanataka kuendelea kuishi katika nchi yao ili kushiriki kikamilifu katika mchakato wa ujenzi wa amani na upatanisho.

Askofu mkuu Mamberti anasema, Baba Mtakatifu Francisko katika matukio mbali mbali anaendelea kuonesha mshikamano wake wa pekee kwa Wakristo na watu wote wanaoteseka huko Mashariki ya Kati kutokana na vita. Anawaalika waamini na watu wenye mapenzi mema kuendelea kusali, ili amani ya kweli iweze kupatikana. Baba Mtakatifu kwa njia ya Baraza la Kipapa linaloratibu Misaada ya Kanisa Katoliki, Cor Unum amepeleka msaada wa kiuchumi kwa ajili ya wananchi wanaoteseka huko Mashariki ya Kati.

Sekretarieti ya Vatican inaendeleza mchakato wa mikakati ya kidiplomasia, ili kuwahamasisha viongozi wakuu wa Jumuiya ya Kimataifa kuyaangalia mateso na mahangaiko ya Wakristo huko Mashariki ya Kati. Ni matumaini ya Vatican kwamba, Jumuiya ya Kimataifa itaguswa na kuanza kushughulikia mateso ya wananchi wa Iraq katika ujumla wao kwani vitendo vinavyofanyika huko Mashariki ya Kati vinagusa utu na heshima ya binadamu na haki zake msingi. Haya ni mambo msingi yanayowawezesha wananchi kuishi kwa amani na utulivu, hata katika tofauti zao msingi.

Askofu mkuu Dominique Mamberti anasema, inasikitisha kuona kwamba, vita inayoendelea huko Mashariki ya Kati imeanza kuzoeleka, lakini watu wakaendelea kuteseka na kupoteza maisha. Baba Mtakatifu Francisko anaendelea kuhamasisha waamini na watu wote wenye mapenzi mema kusali kwa ajili ya kuombea amani huko Mashariki ya Kati. Kuna haja kwa Jumuiya ya Kimataifa kuhakikisha kwamba, vita inasitishwa, amani inatawala kwa ajili ya ustawi na mafao ya wengi, utu na heshima ya binadamu.







All the contents on this site are copyrighted ©.