2014-07-28 09:35:01

Yesu Kristo ndiye hazina iliyofichika!


Baba Mtakatifu Francisko, Jumapili iliyopita tarehe 27 Julai 2014 akiwa kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, alizungumzia mifano iliyotolewa na Yesu kuhusu Ufalme wa Mungu, unaoweza kumfikia mwamini pasi na kutarajia au baada ya kufanya hija ya kipindi kirefu katika maisha, anapogundua hazina hii, anauza kila kitu ili kuweza kuipata.

Hivi ndivyo mambo yalivyo hata katika Ufalme wa Mungu. Kwa mtu anayemfahamu, aliyebahatika kukutana na Yesu, anabaki akiwa amepigwa na bumbuwazi kutokana na unyenyekevu wake, ukweli na uzuri. Hii ni changamoto kwa waamini kumtafuta Yesu kwani Yesu ndiye hazina ile kubwa ambayo imefichika machoni pa wengi. Watakatifu na watu wengi waliobahatika kusoma na kutafakari Injili wamebahatika kumgundua na kukutana na Yesu katika maisha yao, kiasi kwamba, wametubu na kumwongokea Mungu.

Hawa ni kama vile akina Mtakatifu Francisko wa Assis aliyeachana na malimwengu baada ya kukutana na Yesu akagundua Ufalme wa Mungu akaamua kuukumbatia. Yesu anazungumza na mtu kutoka katika undani wake na kumwezesha mwamini kubadili mwelekeo wa maisha yake na kuwa ni mtu mpya zaidi. Kwa mwelekeo huu, mwamini anapata mambo msingi, mwanga na faraja hata katika shida, masumbuko na kifo, changamoto kwa waamini kujenga utamaduni wa kujisomea Neno la Mungu, ili kuweza kukutana na Yesu ambaye ndiye hazina kubwa iliyofichika, ili kumpatia nafasi Mwenyezi Mungu kuweza kutawala katika maisha yao.

Baba Mtakatifu Francisko anawakumbusha waamini kwamba, Mungu ni upendo, ni chemchemi ya amani na furaha kwa wote na huu ndio utashi wa Mungu kwa kila mwanadamu ndiyo maana amemtoa Mwanaye wa pekee Yesu Kristo ili azaliwe, ateswe na kufa Msalabani kwa ajili ya kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti na hivyo kimkirimia maisha ya uzima wa milele. Kumpata na hatimaye kumkumbatia Yesu ni chemchemi ya furaha ya maisha ya Kikristo.

Waamini wanachangamotishwa na Mama Kanisa kuhakikisha kwamba, wanatolea ushuhuda wa imani yao kwa Kristo na Kanisa lake katika uhalisia wa maisha ya kila siku. Baba Mtakatifu anamwomba Bikira Maria awaombee waamini ili Ufalme wa Mungu uweze kufika hapa duniani, Ufalme unaojikita katika upendo, haki na amani.







All the contents on this site are copyrighted ©.