Marehemu Kardinali Francesco Marchisano alijisadaka kwa ajili ya Kristo na Kanisa
lake!
Baba Mtakatifu Francisko amemtumia salam za rambi rambi Askofu mkuu Cesare Nosiglia
wa Jimbo kuu la Torino kutokana na kifo cha Kardinali Francesco Marchisano, aliyefariki
dunia, Jumapili tarehe 27 Julai 2014. Baba Mtakatifu anapenda kuwahakikishia wote
walioguswa na msiba huu uwepo wake wa karibu, katika kipindi hiki cha maombolezo.
Kwa namna ya pekee, Baba Mtakatifu anamkumbuka Marehemu Kardinali Marchisano
aliyejisadaka kwa ajili ya shughuli mbali mbali za kitume mjini Vatican, hasa zaidi
katika Baraza la Kipapa la Elimu Katoliki na baadaye akateuliwa kuwa Mhudumu mkuu
wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican na mwishoni kabisa, alikuwa ni Rais
Idara ya Kazi ya Vatican.
Marehemu Kardinali Marchisano anaacha ushuhuda mkubwa
wa maisha ya kiongozi aliyejitosa kimasomaso kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake, kama
Padre na Askofu, daima akiwa makini kutekeleza mahitaji ya waamini wake, makini katika
utunzaji wa sanaa na utamaduni. Baba Mtakatifu anamwombea Marehemu ili Mwenyezi Mungu
aweze kuipokea roho ya Marehemu katika raha na amani ya milele. Baba Mtakatifu anapenda
kuchukua fursa hii kutoa baraka zake za kitume kwa wote wanaoomboleza kifo cha Kardinali
Marchisano.
Wakati huo huo, Mshereheshaji mkuu wa Ibada za Kipapa, Monsinyo
Guido Marini anasema kwamba, Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya kumwombea Marehemu
Kardinali Francesco Marchisano, itaadhimishwa Jumatano tarehe 30 Julai 2014, majira
ya saa 2:00 za asubuhi kwa saa za Ulaya na kuongozwa na Kardinali Angelo Sodano, Dekano
wa Makardinali. Baba Mtakatifu Francisko anatarajiwa kuongoza Ibada ya Mazishi.