2014-07-28 12:23:26

Chama cha Mtakatifu Anna Jimbo kuu la Mombasa kinaadhimisha kumbu kumbu ya miaka 60 tangu kuanzishwa kwake!


Chama cha Wanawake cha Mtakatifu Anna, Jimbo kuu la Mombasa, Kenya, hivi karibuni kimeadhimisha kumbu kumbu ya miaka sitini tangu kilipoanzishwa kama chombo makini cha Uinjilishaji miongoni mwa Wanawake Wakatoliki, Jimbo kuu la Mombasa.

Ibada ya Misa takatifu katika maadhimisho haya imeongozwa na Padre Boniface Malai aliyekazia dhamana na nafasi ya wanawake wakatoliki katika mchakato wa Uinjilishaji mpya unaopania kuwapatia waamini nyenzo za kuweza kushuhudia imani yao kwa njia ya matendo mema na adili.

Padre Malai ambaye ni Dekano wa Dekania ya Taita, Taveta, Jimbo kuu la Mombasa amewataka wanawake kujifunga kibwebwe ili kushirikiana na mihimili mingine ya Uinjilishaji mpya katika utangazaji wa Injili ya Furaha miongoni mwa watu wa mataifa. Wanawake wanakumbushwa kwamba, wao ni viungo muhimu sana katika kulea na kurithisha imani kwa watoto wao. Wanawake Wakatoliki wakipania wanaweza kulitegemeza Kanisa mahalia katika nyanja mbali mbali za maisha na utume wa Kanisa.

Kumbu kumbu ya Miaka sitini tangu kuanzishwa kwa Chama cha Mtakatifu Anna, zimekwenda sanjari na maadhimisho ya Kumbu kumbu ya Mtakatifu Joakim na Anna, wazazi wake Bikira Maria, iliyoadhimishwa hapo tarehe 26 Julai 2014. Zaidi ya wanawake mia nane kutoka Dekania ya Taita, Taveta walikusanyika pamoja ili kumwimbia Mwenyezi Mungu utenzi wa sifa na shukrani kwa matendo makuu aliyowakirimia katika maisha na utume wao ndani ya Jimbo kuu la Mombasa.

Katika maadhimisho haya wanawake kumi waasisi wa Chama cha Mtakatifu Anna walikuwepo, jambo la kutia faraja na matumaini kwamba, inawezekana watu kuwa waaminifu katika maisha na utume wa Kanisa!

Wakati huo huo, Bibi Felista Kirigha, Mwenyekiti wa Dekania ya Taveta, amewashukuru Mapadre na watawa kwa huduma zao makini kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya Wanawake Wakatoliki Jimbo kuu la Mombasa. Ameitaka Familia ya Mungu Jimbo kuu la Mombasa, kushikamana na kushirikiana kwa pamoja ili kwa pamoja waweze kulijenga Kanisa la Kristo kwa njia ya ushuhuda wa maisha yao.

Wanawake wamekumbushwa kwamba, wanayo nafasi ya pekee kabisa katika kurithisha, kukuza na kulea misingi ya imani, maadili na utu wema. Wanawake wamekuwa mstari wa mbele katika maisha na utume wa Kanisa hasa kwa kushiriki katika Jumuiya ndogo ndogo za Kikristo. Wanawake wanatakiwa kusimama kidete kuwa ni watangazaji makini wa Imani kwa njia ya ushuhuda wa maisha yao, kwa kuendelea kutangaza pia Injili ya Uhai dhidi ya utamaduni wa kifo unaozinyemelea familia nyingi duniani.

Katika Ibada hii ya Misa Takatifu wanachama wapya thelathini na wawili wamepokelewa katika Chama cha Wanawake wa Mtakatifu Anna, ili kuendeleza dhamana ya chama hiki katika maisha na utume wa Kanisa. Ibada hii imehudhuriwa na Mapadre, watawa na waamini walei kutoka Dekania ya Taita, Taveta, Jimbo kuu la Mombasa, Kenya.







All the contents on this site are copyrighted ©.