Abiria waliofariki kwa ajali ya ndege huko Mali wakumbukwa kwa Ibada!
Baraza la Maaskofu Katoliki Burkina Faso, Jumapili tarehe 27 Julai 2014 katika Kanisa
kuu la Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili, Jimbo kuu la Ouagadougou, limeadhimisha
Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya kuwakumbuka na kuwaombea abiria wa Shirika la
Ndege la Algeria iliyoanguka hivi karibuni nchini Mali na hivyo kusababisha vifo vya
abiria 116 waliokuwemo ndani ya ndege hiyo! Ibada hii ya Misa Takatifu imeongozwa
na Kardinali Philippe Ouedraogo, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Ouagadougou, Burkina
Faso.
Katika Ibada hii waamini pia wamewakumbuka na kuwaombea ndugu, jamaa
na marafiki wa abiria waliofariki dunia kwa ajili ya ndege huko Mali na sehemu nyingine
za dunia ambako hadi sasa watu wanaendelea kuomboleza kutoka na majanga ya ajali za
ndege. Ni katika ukimya, watu wanaweza kupata majibu yanayoendelea kusumbua vichwa
vya watu wanapotafakari kuhusu ajali hizi za ndege. Ni Mwenyezi Mungu peke yake anayeweza
kuzima kiu ya mahangaiko ya mwanadamu, changamoto kwa waamini kuendelea kujikita katika
imani na matumaini wakati huu wa maombolezo na msiba mkubwa.