2014-07-26 10:15:59

Wewe ungeomba lini?


Baada ya kutafakari Injili juu ya ngano na magugu Dominika iliyopita, Injili ya leo – inatualika tutafute ilipo hazina na lulu ya kweli. Hapa Yesu Kristo anatamka mwenyewe juu yake na ujio wake ulimwenguni. Hivi tunaalikwa tutumie nafasi hii njema ya wokovu.

Ni muda wa kuamua. Hazina, yaani Kristo, yupo. Tusipoteze nafasi hiyo. Hii mifano miwili hazina na lulu ni mwaliko wa kuutafuta huo ufalme. Tungeweza kujiuliza mara moja – Je, sisi tunatafuta nini au tumewekeza wapi? Katika maisha ya kawaida twaona kuwa tumewekeza sana kaitka mambo mengi kwa mfano kwenye bima ya maisha, ya afya nk. Ni sawa na sahihi kabisa. Na bima hizi huwa ni kwa ajili ya kulinda maisha ya kawaida ya mtu awapo duniani na pengine baada ya kifo wale wanaobaki waweze kupata sehemu ya mali ya marehemu.

Bibi mmoja aliyekuwa tajiri – alipofariki bahati nzuri alifika mbinguni. Ila alipata sehemu ndogo ya kukaa na pembezoni. Akamlalamikia malaika aliyemwongoza kwenda sehemu hiyo. Unanileta mahali hapa? Mbona mimi huko duniani nilikuwa na kila kitu na nilikapaa mahali pa fahari? Malaika kwa unyenyekevu akamjibu – tafadhali ridhika na ulichopata. Vile vifaa vya ujenzi ulivyotuma huku mbinguni vilitosha kutengeneza tu kiti hiki kidogo ambapo ndiyo mahali pako pa kujisetiri milele. Ridhika na ulichotoa. Malaika akaenda zake.

Leo hii tunaalikwa tuwekeze kwenye bima ya ufalme wa mbinguni. Tukumbuke kuwa ufalme wa mbinguni ni bima dhidi ya kifo. Yesu atuambia waziwazi, aniaminiye hata kama akifa, ataishi milele. Hivyo twaelewa vizuri mwaliko wake – uza vyote na kuutafuta kwanza ufalme. Kuwa tayari kutoa sadaka yo yote kwa ajili ya huo ufalme wake.

Leo tunaulizwa – katika yote ninayotamani katika maisha – ni kipi nathamini zaidi au nahitaji zaidi? Injili inaweka wazi– kwanza ufalme wa mbinguni – Mt. 6:33 –basi, kwanza utafuteni ufalme wa Mungu na uadilifu wake, na hayo yote mtaongezewa. Ufalme wa Mungu ni utawala wa Mungu mioyoni mwetu, katika maisha yetu, nyumbani kwetu, katika jamii na katika ulimwengu wetu. Anayepata ufalme wa Mungu amepata yote. Ndiyo maana inalinganishwa na hazina bora iliyopatikana shambani au lulu ya thamani kubwa. Msisitizo uko siyo kutafuta kwanza ufalme wa Mungu pamoja na mengine yanayoambatana nayo lakini msisitizo uko katika kutafuta tu ufalme huo.

Pengine somo la kwanza litupe changamoto tena leo – Sulemani akiwa mfalme kijana alikuwa na mahitaji mengi sana. Alihitaji utajiri, jeshi kubwa na imara, umaarufu, usalama, ustawi, maisha marefu, furaha n.k. Lakini katika nafasi aliyopewa na Mungu ya kuomba – aliomba hekima. Alifahamu fika akiwa na hekima ya Mungu mengine yote yatawezekana. Na Mungu anamhakikishia hilo 1 Waf. 3: 11-13 –Mungu akamwambia, kwa kuwa umeomba jambo hili – wala hukujitakia maisha marefu, wala hukujitakia utajiri, wala hukuomba roho za adui zako, bali umeomba hekima ya kujua kuhukumu, basi, tazama ninatenda kama ulivyosema. Ninakupa moyo wa hekima na akili, hata kabla yako hakupatikana mtu kama wewe, na wala baada yako hatainuka mtu kama wewe,. Hata mambo yale usiyoyaomba nimekupatia: utajiri, heshima na utukufu kushinda wafalme wengine wote.

Sijui leo tungepata nafasi kama ya Mfalme Sulemani tungeomba nini. Utajiri, mafanikio katika biashara? Maisha mema na ya upendo thabiti? Je tungekuwa na hekima ya Sulemani kuomba hekima katika maisha yetu ya kila siku? Ni ipi nafasi ya ufalme wa Mungu katika maisha yako? Tusisahau kuwa ufalme wa Mungu si moja kati ya mambo tuyatamaniyo ila ndicho pekee tunachohitaji. Mengine ni ziada.

TUMSIFU YESU KRISTO.
PD. REGINALD MROSSO, C.PP.S.








All the contents on this site are copyrighted ©.