2014-07-24 15:20:04

Tafakari ya neno la Mungu, Jumapili ya 17 ya Kipindi cha Mwaka A wa Kanisa


Mpendwa unayenisikiliza, Neno la Mungu Dominika ya 17 ya mwaka A, linakualika kuhangaikia na kuchagua jambo lililo la thamani kubwa kuliko mengine yote na jambo hili ni ufalme wa mbinguni. RealAudioMP3
Mfalme Suleimani akiwa amechaguliwa kumrithi baba yake Daudi, anaomba moyo wa adili ili daima atangaze hukumu ya Mungu iliyo ya haki katika utawala wake. Kwa nini mfalme anasali sala hii? Naomba tukumbuke kuwa nyakati za mwisho za utawala wa Daudi zilikuwa za machafuko na upinzani mwingi. Kumbe mfalme Suleimani anapoingia katika madaraka anajikabidhi mikononi mwa Mungu mwenye uweza wa kuyaondoa madhulumu haya katika taifa lake.

Sala ya mfalme Suleimani ni kinyume cha hali ya kawaida na matarajio ya wafalme wengi wa dunia. Ndiyo kusema katika hali ya kawaida tungetarajia mfalme aombe utajiri zaidi, familia kubwa zaidi, uwezo na nguvu za kijeshi ili kushinda maadui, lakini badala yake anaomba hekima ya kimungu itokayo juu. Kwa sala hii Mungu anapendezwa na mfalme na anamjalia hekima ya kimungu itakayomsaidia kutawala taifa lake.

Mpendwa mwana wa Mungu, Mwinjili Matayo anakazia ujumbe huo, anapotuwekea mfano wa mtu mmoja aliyeuza vitu vyake vyote ili aweze kununua kipande cha shamba. Mtu huyu aligundua kuwa kuna kitu cha thamani kubwa katika kipande kile cha shamba alichonunua akilinganisha na mali aliyoiuza. Hakuogopa kwamba kuna uwezekano wa mwenye kuuza kile kipande kubadilisha mawazo na hivi ikawa ni hasara kwake baada ya kuwa amejitosa kwa kuuza vitu vyake vyote.

Mtu huyu pia hachelewi maana anaona muda ni wa maana na akikosea atapoteza kila kitu. Mara moja hapa nakumbuka lile neno lisemalo mtumikieni Bwana Mungu wako ungali ukiwa kijana kabla hazijaja siku za uzee! Mwaliko ni kuchangamkia maisha ya imani mapema pasipo kuweka mashaka katika maisha yako.

Je, ni kitu gani mwinjili anataka kutuambia? Kwa hakika ni hazina ya imani, ni hazina ya Sakramenti, ni hazina ya mapendo, ni hazina ya kuwa mwanajumuiya wa Kanisa Moja, Takatifu, la Kitume na Katoliki. Kwa ujumla ni kuunganika na Mungu mwenyewe aliyejifunua kwetu kwa njia ya umwilisho wa Mwanae wa pekee.

Ndiyo kusema kama ukimchagua Mungu, mtume Paulo anasema daima Kristu mzaliwa wa kwanza atakuja kwako na kukupa mema yote ya kiroho na utahesabiwa haki mbele ya Mungu. Mpendwa hiyo ndiyo hazina anayotufundisha mwinjili, ndiyo hekima na adili ambayo mfalme Suleimani anaitafuta na kuiomba mbele ya Mungu. Nasi tuombe hekima ya kimungu daima katika maisha yetu tukikumbuka kanuni ya mlimani yaani “heri walio maskini wa roho maana ufalme wa mbinguni ni wao! Tumsifu Yesu Kristo.

Tafakari hii imeletwa kwenu na Padre Richard Tiganya C.PP.S.








All the contents on this site are copyrighted ©.