Nchini Burundi katika kipindi cha miaka ishirini, idadi ya madhehebu ya kidini nchini
humo imeongezeka maradufu kutoka madhehebu arobaini na tano hadi kufikia madhehebu
mia sita, kiasi cha kuihamasisha Serikali ya Burundi kutafuta njia ya kudhibiti wimbi
hili kubwa kwa kutunga sheria ambayo tayari imepitishwa na Bunge la Burundi.
Ili dhehebu
la kidini liweze kutambulika rasmi kisheria nchini Burundi, halina budi kuwa na wafuasi
walau mia tano na kama dhehebu hili linatoka nje ya nchi basi linapaswa kuwa na wafuasi
walau elfu moja. Madhehebu ya dini nchini Burundi yamepewa kipindi cha miaka miwili,
ili kuweza kurekebisha kasoro zilizopo na hatimaye, sheria iweze kuanza kushika mkondo
wake, ili kudhibiti ongezeko la madhehebu ya kidini ambayo mengi yameonesha kuwa na
msukumo wa kiuchumi zaidi, kuliko hata maisha ya kiroho.
Wachunguzi wa masuala
ya kidini wanasema, kufumuka kwa amdhehebu haya kunawawezesha viongozi wake kuendelea
kupata msaada wa raslimali fedha na hivyo kugeuza madhehebu haya kuwa kweli ni vitega
uchumi na hivyo hata kushindwa kudhitiwa na Serikali. Takwimu zinaonesha kwamba, aslimia
75% ya wananchi wa Burundi ni waamini wa Kanisa Katoliki na kwamba, asilimia kati
ya 3-4% ni waamini wa dini ya Kiislam na wengine waliobakia ni waamini wa Madhehebu
mbali mbali ya Kikristo.
Wachunguzi wa mambo wanasema, sheria hii imekuja wakati
ambapo Burundi inajiandaa kwa ajili ya kuanza mchakato wa uchaguzi mkuu unaotarajiwa
kufanyika nchini humo kunako mwaka 2015. Madhehebu ya kidini yanaweza kuwa ni mwiba
mkubwa katika mchakato wa uchaguzi huu ukitazamwa kwa jicho la kisiasa. Bado watu
wanakumbuka mauaji ya waamini wa madhehebu ya Kikristo yaliyofanyika kunako mwaka
2013, mjini Businde, Mkoani Kayanza.
Wizara ya mambo ya ndani ya Burundi inasema
kwamba, lengo la sheria hii ambayo imepitishwa hivi karibuni nchini Burundi ni kudhibiti
wimbi la madhehebu ya kidini pamoja na kuimarisha ulinzi na usalama kwa wananchi wa
Burundi. Ibada za madhehebu haya zinapaswa pia kufanyika katika maeneo yenye hadhi
ya Ibada kwa ajili ya kumtukuza Mwenyezi Mungu na mwanadamu kutakatifuzwa. Imani ni
chaguo la mtu binafsi na kwamba, uhuru wa kidini hauna budi kuheshimu pia haki msingi
za wananchi wengine ndani ya Jamii.