Mama Meriam kutoka Sudan akutana na Papa Francisko mjini Vatican
Baba Mtakatifu Francisko, siku ya Alhamisi mchana tarehe 24 Julai 2014 amekutana na
kuzungumza na Mama Meriam Ibrahim Ishag, mwanamke Mkristo kutoka Sudan aliyehukumiwa
adhabu ya kifo na hatimaye adhabu hii kubatilishwa na mahakama ya rufaa nchini Sudan
hivi karibuni. Katika mazungumzo haya, Meriam alikuwa ameambatana na mme wake Daniel
Wani pamoja na watoto wao wawili.
Mtoto wao mdogo anayeitwa Maya alizaliwa
gerezani miezi miwili iliyopita. Familia hii imesindikizwa na Waziri mdogo wa mambo
ya nchi za nje wa Italia Lapo Pistelli, ambaye alikuwa nchini Sudan, ili kukamilisha
taratibu na mipango ya kuachiliwa huru kwa Mama Meriam kutoka Sudan ambaye pamoja
na familia yake wanatarajiwa kwenda kuishi nchini Marekani.
Baba Mtakatifu
na wageni wake wameweza kufanya mazungumzo yaliyodumu kwa takribani nusu saa kwenye
Hosteli ya Mtakatifu Martha, iliyoko mjini Vatican. Baba Mtakatifu amemshukuru Meriam
na familia yake kwa ushuhuda wa imani ya Kikristo waliyoionesha. Kwa upande wake,
Meriam amemshukuru Baba Mtakatifu na watu wote wenye mapenzi mema waliowasindikiza
kwa sala na majitoleo yao hadi kuachiliwa huru.
Mwishoni, Baba Mtakatifu amezungumza
na viongozi wa Italia waliokuwa wamemshindikiza Mama Meriam na familia yake, ili kukutana
na kuzungumza na Baba Mtakatifu Francisko. Baba Mtakatifu ameonesha kuguswa na wote
wanaoteseka kutokana na imani yao au ukosefu wa uhuru wa kidini, hasa zaidi kwa Wakristo
kutoka sehemu mbali mbali za dunia.